• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
Mama ‘mafichoni’ baada ya kulipwa fidia ya ujenzi wa bwawa la Kariminu

Mama ‘mafichoni’ baada ya kulipwa fidia ya ujenzi wa bwawa la Kariminu

Na LAWRENCE ONGARO

FAMILIA moja katika kijiji cha Buchana, Gatundu Kaskazini, inaiomba serikali kuingilia kati baada ya mzazi kwenda mafichoni na pesa alizopata za fidia ya kipande cha ardhi ambacho kilichukuliwa kitumike katika ujenzi wa bwawa la Kariminu.

Bi Nancy Njoki, 60, alitoweka baada ya kulipwa fidia ya Sh11 milioni ili ahamie kwingineko.

Inadaiwa ni miezi miwili sasa tangu mama huyo wa watoto wanne atoroke kutoka kwake.

Bi Njoki ni miongoni mwa wakazi 246 kutoka eneo la Gatundu Kaskazini waliolipwa fidia na Tume ya Ardhi Nchini (NLC).

Kikundi hicho tayari kimelipwa jumla ya Sh1.28 bilioni kama fidia ili wakazi hao wahamie kwingineko ili kupisha mradi huo wa bwawa.

Kulingana na mwanawe mwanamke huyo, Bw Gerald Mungai, mamake aliwasilisha stakabadhi za shamba lao lenye ukubwa wa ekari tatu na nusu kwa NLC.

“Sisi wanawe tulishtuka kupata ya kwamba amekwenda mafichoni ili aponde fedha hizo peke yake,” alisema Bw Mungai.

Hata hivyo, inadaiwa alinunua kipande cha ardhi cha kiasi cha ukubwa wa 40 by 80 mraba kwa kiasi cha Sh50,000.

“Sasa mama anataka sisi wanawe wanne tukaishi huko ambako hakuna maji wala umeme na ni kukavu ajabu,” alisema Bw Mungai ambaye ndiye kijana mkubwa katika familia hiyo.

Alisema babake mzazi alifariki zamani na kwa hivyo walibaki na mama mzazi.

Alisema wamebaki kwenye mataa na imebidi watafute nyumba ya kukodisha katika kituo cha biashara cha Buchana, Gatundu.

“Sasa tumerejea katika maisha ya upweke kwani tunatafuta kazi za vibarua ili tujikimu kimaisha. Tunaiomba serikali kuingilia kati ili itusaidie kutatua jambo hilo,” alisema Bw Mungai.

Kijana mwingine wa familia hiyo, Bw Francis Kinyua, alisema tayari wamepiga ripoti kwa kituo cha polisi lakini hakuna chochote kimetekelezwa.

Alisema tayari mamake amewatisha akisema ya kwamba wakiendelea kulalamika atachukua hatua wakamatwe na washtakiwe kwa sababu yeye ndiye mwenye shamba hilo.

Watu wachache wanatarajia kupokea fidia zao baada ya kuambiwa wangoje.

Wengine ilidaiwa wana shida za migogoro ya hapa na pale kuhusu umiliki wa vipande vya ardhi.

You can share this post!

Forlan astaafu rasmi kucheza soka ya dunia

‘Sultan’ aburudika majuu magenge yakihangaisha...

adminleo