• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Gavana ataka wabunge warejeshe mamilioni ya ziara ya Amerika

Gavana ataka wabunge warejeshe mamilioni ya ziara ya Amerika

Na SIMON CIURI

GAVANA wa Machakos, Dkt Alfred Mutua anataka wabunge walazimishwe kurejesha mamilioni ya fedha za umma walizotumia katika ziara ya Amerika.

Dkt Mutua, aliyekuwa akizungumza katika jumba la kibiashara la Spur Mall, Ruiru, katika Kaunti ya Kiambu, alisema ziara hiyo haina manufaa kwa Wakenya, hivyo wabunge ni shati walazimishwe kurejesha fedha hizo.

“Idadi kubwa ya wabunge walioelekea nchini Amerika ni ithibati kwamba walikuwa wameenda likizo. Ziara hizo zisizokuwa na manufaa kwa walipa ushuru ndizo zimefanya gharama ya kuendesha mabunge ya kaunti kuwa juu,” akaongezea.

Gavana Mutua aliwataka viongozi kuzingatia agizo la serikali iliyopiga marufuku idadi kubwa ya watu kuhudhuria kongamano moja.

“Kuna sera ya serikali inayodhibiti idadi ya watu wanaofaa kuhudhuria kongamano moja. Inasikitisha kwamba serikali za kaunti tuliandikiwa barua tukitakiwa tusitume zaidi ya watu watatu katika kongamano ilhali bunge linatuma zaidi ya watu 60,” akasema kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap.

Mbali na wabunge, wengine waliosafiri ni maseneta, madiwani na wafanyakazi wa bunge.

Inakadiriwa kuwa Wakenya walipoteza zaidi ya Sh100 milioni katika ziara hiyo.

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga tayari ameshutumu ziara hiyo akisema kuwa ni uharibifu wa fedha za walipa ushuru.

Dkt Mutua, wakati huo huo, alitangaza kuwa atazindua kituo cha kutafiti maradhi ya kansa katika Kaunti ya Machakos.

“Tutatumia Sh100 milioni na baadaye tutaongezea Sh300 milioni kuhakikisha kuwa kituo hicho kitakuwa na vifaa vyote vinavyohitajika. Wakazi watapimwa kansa bila malipo,” akasema Gavana Mutua.

You can share this post!

Aliyejiua kuhusu kansa alihofia upasuaji – Familia

Hofu mgomo wa watumishi wa kaunti ukinukia

adminleo