• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Vijana tumieni vyema Sh200 bilioni za serikali kujinufaisha – Wamalwa

Vijana tumieni vyema Sh200 bilioni za serikali kujinufaisha – Wamalwa

Na BERNARDINE MUTANU

WAZIRI wa Ugatuzi na Maeneo Kavu (ASALS) Eugene Wamalwa Alhamisi amewahimiza vijana kutwaa nafasi zilizotolewa na serikali kujiimarisha kimapato.

Alisema kuwa vijana ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu, hivyo walihitajika kuhusishwa katika masuala makuu nchini.-

Wakati wa warsha ya vijana kutoka Eneo la Maziwa Makuu (ICGLR), Nairobi, waziri huyo alisema kulikuwa na haja kubwa ya kuwahusisha vijana kwa kuwaundia nafasi katika jamii kwa kuwazuia kujiingiza katika mambo ya kihalifu kama vile ugaidi.

Hata hivyo, alilalamika kuwa licha ya serikali kutoa kima cha Sh200 bilioni kuwasaidia vijana, ni wachache tu ambao wametumia nafasi hiyo kujinufaisha.

“Inasikitika kwamba licha ya serikali kutoa Sh200 bilioni, ni vijana wachache sana ambao wametumia hudumu hiyo. Fedha zilizochukuliwa sio zaidi ya Sh50 bilioni. Vijana wanafaa kutumia nafasi hiyo kujinufaisha,” alisema.

Kulingana na Bw Wamalwa, mkataba uliotiwa sahihi Rwanda wa kufungua eneo la Afrika majuzi utakuwa wa manufaa makubwa kwa vijana kwani watakuwa na uwezo wa kufanya kazi na kuanzisha biashara eneo lolote Barani Afrika.

Waziri huyo alisema vijana ni kiungo muhimu katika ajenda ya maendeleo ya serikali, “Ikiwa hatutaweka vijana katikati mwa ajenda ya maendeleo, itakuwa vigumu kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs),” alisema waziri huyo.

Alisema wizara yake itafadili vijana kufikia 300 katika warsha ijayo ya magavana mjini Kakamega, kwa lengo la kuchukua maoni yao kuhusu baadhi ya masuala nchini.

Kulingana na wataalam waliohudhuria warsha hiyo, ukosefu wa ajira kwa vijana umesalia changamoto kuwa kubwa zaidi katika kufanikisha amani Eneo la Maziwa Makuu.

Hii ni kutokana na kuwa kutokana na changamoto hiyo, vijana wengi huingia katika makundi yasiyofaa kama vile ya kigaidi.

“Ukosefu wa ajira una uwezo wa kudhoofisha uchumi wa taifa na pia unaweza kuyumbisha taasisi au kuzua vurugu,” alisema Katibu Mkuu wa ICGLR Bw Zachary Muburi Muita wakati wa warsha hiyo ya siku moja.

Alisema katika mataifa mengi ikiwa vijana hawatahusishwa katika ajenda ya maendeleo, wataingia katika uhalifu.

You can share this post!

Waangalizi wa uchaguzi walitishwa na kuuawa, Elog yasema

Mwanasheria Mkuu mpya mtarajiwa aahidi kutatua janga la...

adminleo