Facebook yashtakiwa huku thamani yake ikishuka kwa kuruhusu Cambridge Analytica kudukua akaunti
Na REUTERS na CHARLES WASONGA
FACEBOOK na kampuni ya kutoa ushauri wa kisiasa ya Cambridge Analytica zimeshtakiwa nchini Amerika kwa kutoa habari za siri za zaidi ya watu 50 milioni wanaotumia huduma za mtandao huo wa kijamii, bila idhini yao.
Kesi hiyo iliyowasilishwa Jumanne jioni na Lauren Price, mkazi wa Maryland, ni ya kwanza dhidi ya Facebook kutokana na kutomakinika kwake kulinda data za wateja wake.
Pia ni kesi ya kwanza dhidi ya kwa kutumia data hiyo, bila idhini, kwa ajili ya kupiga jeki kampeni za Rais Donald Trump katik kampeni za kuelekea uchaguzi wa Novemba 2016.
“Kila mtumiaji mtandao wa Facebook ni mhusika katika kesi hii kwani data zao zilitwaliwa bila idhini yao. Kwa hivyo, haki yao ya usiri imeingiliwa,” John Yanchunis, ambaye ni wakili wa Price, alisema kwenye mahojiano kwa njia ya siku Jumatano.
Kesi hiyo imewasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya San Jose, jimboni California, Amerika.
Iliwasilishwa saa kadhaa baadaya Facebook kuelekezewa lawama katika kesi nyingine iliyowasilishwa na mwenyehisa mmoja aliyedai bei ya hisa zake zilishuka baada ya sakata hiyo kufichuliwa. Kesi hiyo ya pili iliwasilishwa katika mahakama ya San Francisco.
Bei ya hisa za Facebook ilipungua kwa takriban dola 50 bilioni (Sh5 bilioni) kwa kipindi cha siku mbili pekee.
Hadi tulipokuwa tukienda mitamboni, Facebook na Cambridge Analytica (yenye makao yake jijini London) hazikuwa zimetoa kauli zao kuhusu tuhuma hizo.
Bi Price anazisuta Facebook na Cambridge Analytica kwa kutokamikinika na kukiuka sheria kuhusu ushindani sawa unaotumika jimboni California.
Alisema Facebook ilikiuka sera yake kuhusu usiri kwa kutoa maelezo/data za wateja wake bila idhini yao.
“Mteja wetu alikuwa akipata jumbe za kisiasa katika ukurasa wake wa facebook wakati wa kipindi cha kampeni. Hukuwa amewahi kuona jumbe kama hizo wakati mwingine,” Yanchunis akasema.
“Hakuelewa kilichokuwa kikiendelea wakati huo lakini saa ameng’amua kuwa jumbe hizo zilenga kumshawishi kupitia upande kura kura.
Mlalamishi anataka kulipwa ridhaa ya kiwango ambacho hakutaja, pamoja na adhabu kali kwa Facebook na Cambridge Analytica.