Habari Mseto

KNH mashakani tena kufuatia upasuaji ovyo wa utumbo

March 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Eneo la matibabu ya dharura katika Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi. Picha/ Maktaba

Na BENSON MATHEKA

HOSPITALI Kuu ya Kenyatta imejipata mashakani tena kufuatia madai kwamba mwanamke aliyekuwa akijifungua kupitia upasuaji aliathirika baada ya kupasuliwa visivyo.

Mwanamke huyo, Susan Nekesa anasema alifika katika hospitali hiyo Januari 25 na akajifungua siku iliyofuata.

Hata hivyo saa kadhaa baada ya upasuaji, tumbo lake lilivimba na akapata maumivu makali.

Akiongea na runinga ya Citizen Jumatano, mwanamke huyo alisema maumivu yalimzidi akashindwa kuongea.

Kwenye mahojiano na runinga hiyo Nekesa alionekana akitatizika kuketi kitandani huku akitokwa machozi na kusema anachoomba ni asipoteze uwezo wa kukumbuka mambo.

“Nilipokuja kumuona, nilipata tumbo lake likiwa limevimba. Tumbo lilikuwa na joto sana na hangeweza kuongea,” dadake Evelyn Anindo, alisema.

Alipolalamikia hospitali ya KNH, Nekesa alirudishwa katika chumba cha upasuaji na madaktari wakakiri kwamba walikuwa wamefanya makosa.

“lligunduliwa kuwa upasuaji haukuwa umefanywa vyema,” alisema Robert Sitati, mume wa Nekesa.

“Sehemu ya utumbo wake, yaani sentimita 50 ilikuwa nje ya unapopaswa kuwa,” alisema.

Ili kurekebisha hali, madaktari walitoa sehemu iliyoathiriwa na kuacha shimo ndogo

( inayofahamika kama stoma) ili aweze kupitishia choo kupitia mfuko. Familia yake iliomba aweze kupona  ili aruhusiwe kwenda nyumbani na watoto wake pacha.

Hata hivyo, mnamo Jumanne familia ilifahamishwa kuwa mmoja wa watoto hao alikuwa amekufa.

 “Walisema mtoto wangu alikuwa na tundu kwenye roho,” alisema Nekesa kwa uchungu.

Hata hivyo, mumewe alisema alifahamishwa na mfanyakazi wa KNH kwamba mtoto huyo alilishwa na mtu asiyekuwa na ujuzi wa kulisha watoto akasakamwa na maziwa kooni.

Huku akiendelea kuomboleza kifo cha mtoto wake, Nekesa anakabiliwa na wakati mgumu na uchungu kwa madaktari anaodai wamempuuza hata baada ya kusababishia hali hiyo.

 “Hakuna anayemshughulikia,” alisema Evelyn.

Baada ya mfuko anaotumia kupitishia choo kujaa, ni yeye anayeng’ang’ana kwenda chooni kutupa uchafu.

Familia yake imechanganyikiwa huku hospitali ikiwafahamishwa kuwa haina wataalamu wa kumhudumia  na kuwataka wawe na subira.

Sitati anasema hospitali imemuonya dhidi ya kumhamishia mkewe hospitali nyingine .