Wanaounganishia raia umeme kwa njia za mkato waonywa
Na OSCAR KAKAI
WAZIRI Msaidizi wa Kawi, Bw Simon Kachapin amewaonya maafisa katika sekta ya kawi dhidi ya kujihusisha na ufisadi katika usambazaji umeme. Bw Kachapin alisema kuna baadhi ya maafisa katika sekta hiyo ambao wanaunganishia wateja stima kinyume cha sheria.
Alisema kuwa hatua hiyo ni uhalifu wa kiuchumi na yeyote atakayepatikana ataadhibiwa kisheria.
Kulingana naye, hali hii pia husababisha iwe vigumu kutoa huduma za usambazaji umeme ipasavyo kwa wananchi.
“Mtandao wa kusambaza umeme huzidiwa nguvu kw a vile hubeba watu wengi kupita kiasi. Wateja ambao huwa hawalipii stima wanaiharibu na hii ni kuharibu mali,” alisema.
Bw Kachapin alisema hali hii ikikomeshwa pamoja na uharibifu wa vifaa vya usambazaji umeme, itasaidia kuimarisha usambazaji wa stima kwa taifa lote.
Akiongea mwishoni mwa wiki katika kituo cha kibiashara cha Kapsangar, kwenye mpaka wa Kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet, wakati wa kuzindua taa za mitaani kwa lengo la kuunganisha jamii hizo mbili, Bw Kachapin aliwahimiza wakazi kupiga ripoti kuhusu uhalifu wowote unaohusiana na usambazaji umeme.
Kulingana naye, uhalifu aina hiyo huwa pia ni hatari kwa maisha ya wananchi.
“Laini za stima ambazo zimeunganishwa kiholela ni hatari kwa wale wanatumia kwa sababu hazijawekwa kulingana na utaratibu ufaao na kiwango bora,” alisema.
Alisema wakati mwingi majanga yanapotokea yakisababishwa na uhalifu wa kuunganisha umeme kiharamu, serikali ndiyo hulaumiwa ilhali wahusika ni watu binafsi.
“Uhalifu huu hufanywa na watu binafsi kisha kampuni ya Kenya Power inalaumiwa. Tumeanza msako na tunataka umma kutusaidia,” alisema.
Wakati huo huo, waziri huyo msaidizi alionya maafisa husika dhidi ya uzembe na utendakazi duni akisema kuwa lengo la serikali ya Jubilee ni kupeana huduma bora ili mlipa ushuru awe na imani nayo.