Museveni na Kagame waridhiana
Na AFP
MARAIS wa Rwanda na Uganda wametia saini makubaliano ya kusitisha uhasama kati ya mataifa hayo ambao umekithiri kwa miezi kadha.
Mkataba huo ulitiwa saini Jumatano jijini Luanda, Angola, katika sherehe iliyoshuhudiwa na marais Joao Lourenco (Angola), Felix Tshisekedi (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC) na Denis Sassou Nguesso (Congo Brazaville)
Rais Paul Kagame na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni – ambao zamani walikuwa marafiki – wamekuwa wakilumbana huku kila mmoja akidai mwenzake anaingilia masuala ya ndani ya taifa lake.
Wakati mmoja Museveni alimsuta Kagame kwa kuwadhamini wapiganaji ambao wamekuwa wakisababisha mapigano kaskazini mwa Uganda, dai ambalo Kagame alipuuzilia mbali.
Lakini kwenye taarifa ya pamoja waliotoa baada ya kutia saini mkataba huo, viongozi hao wawili walikubaliana “kutojihusisha na vitendo vya kuhujumiana na kupanga kuvuruga amani ndani ya himaya ya kila taifa la kila mmoja kupitia ufadhili na mafunzo ya makundi ya wapiganaji.”
Baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo, Kagame alisema hatarajii kwamba shida yoyote itatokea katika “wakati nitakaofanya kazi pamoja na Rais Museveni kutekeleza yale tumekubaliana kushughulikia.”
“Mkataba huu (MoU) unashughulikia masuala haya yote vizuri na sidhani tutakuwa tukiteua na kuchagua kile ambacho tutatekeleza au kila hatutatekeleza. Tutashughulikia matatizo haya yote. Kwa kufanya hivyo, bila mapendeleo, tutafika mahala tunataka,” akasema Kagame akasema, dakika chache baada ya kuweka sahihi yake katika mkataba huo.
Naye Rais Museveni alisema makubaliano hayo utayasaidia mataifa hayo mawili kustawi kisiasa, kijamii na kiuchumi.
“Tumekubaliana kuhusu masuala ambayo yatatekelezwa kati ya mataifa yetu mawili ambayo yataimarisha usalama wetu, biashara na mahusiano ya kisiasa. Uganda imejitolea kikamilifu kutekeleza mkataba huu,” akasema Museveni.
Rais wa Angola, Lourenco alipongeza mkataba huo akisema unaonyesha kuwa viongozi hao wawili “wako tayari kukomesha uhasama na uadui.”
Biashara kati ya Uganda na Rwanda ilikatizwa tangu Februari mwaka huu, Rwanda ilipofunga mpaka wake eneo la kaskazini, hali iliyoathirika hali ya uchumi katika maeneo yanayopakana huo.
Na mnamo Mei polisi wa Uganda waliwakashifu wanajeshi Rwanda kwa kuingia nchini na kuwaua wanaume wawili. Hata hivyo, Rwanda ilikana madai hayo.
Na mnamo Machi, Rwanda iliikashifu Uganda kwa madai kuwa iliwateka nyara raia wake kando na kuwasaidia waasi ambao wamekuwa wanapanda kupindua serikali hiyo (ya Kagame).
Museveni amewahi kukubali kuwa amekutana na waasi wanaopinga Kagame, lakini akakana madai ya kuunga mkono vitendo vyao (waasi).