Afisa wa sensa anaswa kwa kuiba pombe ya watalii
Na WAANDISHI WETU
SHUGHULI ya kuhesabu watu iliendelea kukumbwa na visanga Jumatatu huku mmoja wa maafisa wa sensa akinaswa kwa kuwaibia watalii pombe hotelini.
Afisa huyo wa sensa aliyetambuliwa kama Antony Kantai, anadaiwa kuwaibia watalii pombe na bidhaa zingine za thamani ya Sh200,000 katika hoteli ya Angama Lodge iliyoko Mbuga ya Masai Mara, Kaunti ya Narok.
Kulingana na polisi, mshukiwa alienda kuhesabu wafanyakazi hotelini hapo kabla ya kuingia katika hema la watalii na kuiba fedha, darubini, tableti, chupa nne za pombe na shuka mbili.
Mshukiwa anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Lolgorian kusubiri kufikishwa mahakamani leo.
Katika Kaunti ya Nakuru, mwanamke alishtakiwa kwa kuchuuza pombe wakati wa sensa.
Katika Kisii na Nyamira, maafisa wa Sensa wameamua kuendesha shughuli ya kuhesabu watu mchana kutokana na hofu ya kukumabana na wachawi usiku.
Katika Kaunti ya Kisumu polisi wanazuilia watu wawili wanaoshukiwa kubaka afisa wa sensa katika eneo la Maseno.
Nao mume na mkewe walikamatwa kwa kuzuia maafisa wa sensa katika mtaa wa Nyalenda kufanya kazi yao.
Katika Homa Bay, afisa wa Sensa katika eneo la Gwassi alisimamishwa kazi baada ya kuacha kuhesabu watu na kwenda kufanya biashara ya boda boda.
Jijini Nairobi kulikuwa na kizaazaa katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba baada ya familia moja kukataa kuhesabiwa Jumapili jioni.
Nao wanawake zaidi ya 1,000 kutoka Tanzania walioolewa na Wakenya katika eneo la Taveta, Kaunti ya Taita Taveta wana matumaini ya kupata vitambulisho baada ya zoezi la sensa.
Katika Kaunti ya Nyandarua wakazi walilalamika kuwa wengi wao hawajahesabiwa licha ya shughuli hiyo kuanza siku tatu zilizopita.
Ripoti za George Sayagie, Lucy Mkanyika, Waikwa Maina, Joseph Openda, Dominic Magara, Sammy Kimatu, Rushdie Oudia, Benson Ayienda, Donnah Atola, Vitalis Kimutai, George Odiwuor Na Shaban Makokha