Habari MsetoSiasa

ODM yaahirisha mchujo, yadai sensa imelemaza mipango

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kinachoongozwa na kinara wa upinzani Bw Raila Odinga kimeahirisha kura ya mchujo ya kuteua mgombeaji wake katika uchaguzi mdogo wa Kibra ambao ungefanyika Jumamosi kutokana na wasiwasi kuhusu hali ya usalama.

Kwenye ujumbe kupitia Twitter, Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho ilisema Jumatano jioni kwamba imeahirisha shughuli hiyo hadi Septemba 7 kutokana na shughuli za sensa.

“NEB imeahirisha mchujo wa kuteua mgombeaji wa chama katika uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Kibra kutokana na kutokuwepo kwa usalama wa kutosha kufuatia sensa inayoendelea,” ikasema.

Wagombeaji 11 walikuwa wameidhinishwa kung’ang’ania tiketi ya ODM katika mchujo huo.

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa mawasiliano wa chama hicho Philip Etale, idadi ya wagombeaji hao ilipungua kutoka 20 baada ya baadhi yao kukosa kutimiza sheria ya masharti yaliyowekwa na ODM.

Wale waliodhinishwa kushiriki mchujo huo ni; Awino Christone Odhiambo, Orero Peter Ochieng’ Sine, Tony Ogola Sira, Ojijo Reuben William, Ayako Oguwa, Stephen Okello Okoth, Bernard Otieno Obayi na Obaricks Eric Ochieng.

Wengine; Owino Brian Shem, Millar John Otieno, Musungu Benson na Owade Lumumba Patrick.

Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha Ken Okoth kutokana na kansa ya utumbo mnamo Julai 26 katika Hospitali ya Nairobi.