Wazee wateta kunyimwa hela kwa sababu ya vidole chakavu
Na FADHILI FREDRICK
BAADHI ya wazee wanaofaidika kutokana na mpango wa pesa kila mwezi kupitia mpango maalum wa serikali kutoka kaunti ya Kwale wamelalamikia kukosa fedha hizo kutokana na uchakavu wa vidole vyao unaosababibishwa na madhara ya kuzeeka.
Wazee hao wamechoshwa na hali hiyo na wametoa wito kwa mawakala wa benki waliopewa kandarasi ya kuwapa pesa kutafuta mbinu mbadala ili wapate pesa hizo bila kuhangaishwa.
Walisema hayo siku ya Jumamosi wakati wa kuwasilisha malalamishi yao kwa Kamati ya Bunge la kitaifa la Leba na Ustawi wa Jamii.
Kamati hiyo iko katika ziara ya kaunti za Pwani ili kutathimini maendeleo ya mpango wa uhamisho wa fedha wa Inua Jamii.
Katibu Mkuu wa Ulinzi wa Jamii, Bi Susan Mochache, alisema kwamba malipo ya wazee yatafanywa kupitia akaunti za benki za walengwa kutoka Oktoba mwaka huu ili kukabili changamoto zinazojitokeza katika mpango huo.
“Serikali bado inafanya kazi ya kuboresha mpango huo ili kuhakikisha kuwa matokeo yake yanafaa kwa watu wake,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati hio Bw Ali Wario na pia Mbunge wa Bura alisema kuwa watajumuisha ripoti kulingana na matokeo yao kutoka ziara ya majimbo ya Pwani kwa lengo la kuhakikisha mpango huo umeboreshwa ili kukidhi mahitaji ya makundi yaliyotekelezwa katika jamii.
“Madhumuni ya ziara hii ni kuthathimini maendeleo na changamoto zinazotokana na mradi huo kwa wazee ili kutafuta mbinu za kuuboresha,” alisema Bw Wario.
Wazee hao walieleza faida wanazozipata kupitia mpango huo wa kijamii na kuipongeza serikali kwa kuwajali.
Hata hivyo, waliiomba serikali kuzingatia kuongeza fedha kutoka Sh2,000 hadi Sh4,000 wakisema gharama ya maisha imepanda.
“Tunathamini msaada wa serikali lakini tunahimiza kufikiria kulipa zaidi kwa sababu kile tunachopata sasa ni kidogo sana ili kukidhi mahitaji yetu yote,” alisema Bw Salim Mwariko wa miaka 72.