• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Nyumba 60 zateketea Mukuru-Kayaba

Nyumba 60 zateketea Mukuru-Kayaba

Na SAMMY KIMATU

FAMILIA zaidi ya 50 zilikesha nje penye baridi baada ya moto mkubwa kuteketeza nyumba 60 Jumatatu usiku.

Moto huo, katika eneo la Mandazi Road lililoko mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba kwenye eneobunge la Starehe, Kaunti ya Nairobi, ulianza mwendo wa saa mbili na nusu usiku.

Inadaiwa ulianzia katika nyumba moja kabla ya kusambaa kwa kasi hadi nyumba zingine kutokana na wenyeji kujiunganishia stima kiholela.

Kulikuwa na hali ya taharuki baada ya vijana wenye hasira kutupia mawe wafanyakazi wa Serikali ya Kaunti wanaozima moto kwa kudai walichelewa.

Mwathiriwa, Bw Elias Ndereva, 35 anayemiliki nyumba mbili alisema aliachwa na kitanda cha wanawe baada ya waporaji kuchukua vitu vyote katika nyumba zake.

Mkazi mwingine, Winnie Nyambura, 23, mama wa mtoto mmoja alisema amebakia na nguo aliyoivalia wakati wa mahojiano na hana mbele wala nyuma.

“Naiomba serikali itusaidie pamoja na mashirika, makanisa au wasamaria wema kwa jumla tunapojizatiti kuanza maisha upya,” akasema Bi Nyambura.

Moto huo ulizimwa kabisa mwendo wa saa nne za usiku pale baada ya kusambaa ulizuiliwa na ua wa kampuni zinazopakana na mtaa huo.

You can share this post!

Kitany: Nimempoteza bavyaa

Mbunge akamatwa kwa kuongoza maandamano msituni Mau

adminleo