• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Ripoti yafichua dawa za Sh15 milioni zimeharibikia hospitalini

Ripoti yafichua dawa za Sh15 milioni zimeharibikia hospitalini

Na IRENE MUGO

MPANGO wa Serikali wa Afya kwa Wote unakabiliwa na changamoto katika kaunti ya Nyeri baada ya kubainika kuwa dawa za thamani ya Sh15 milioni zimepitisha muda wa matumizi katika vituo 13 vya afya eneo hilo.

Kamati ya Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) pia ilisema kuwa bidhaa nyinginezo za thamani ya Sh771,143 pia zimepitisha muda wa matumizi bila maelezo kutolewa kuhusu suala hilo.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa katika bunge la kaunti ya Nyeri ili ijadiliwe na kupitishwa, dawa hizo zilinunuliwa nyingi kupita kiasi kilichohitajika.

“Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu ni kwa nini zilinunuliwa nyingi kupita kiasi, hali iliyofanya nyingi kupitisha muda wa mutumizi. Hii ina maana kuwa pesa za umma ziliharibika bure,” ikasema ripoti hiyo.

Kamati hiyo ilifanya ukaguzi wake katika vituo husika vya afya mnamo Desemba mwaka jana.

Haya yanajiri wakati ambapo wagonjwa wanalazimishwa kununua dawa katika maduka yaliyoko nje ya hospitali husika.

Kaunti ya Nyeri ni miongoni mwa kaunti nne ambako utekelezaji wa mpango wa afya kwa wote ulitekelezwa kwa njia ya majaribio kutokana na hali kwamba huathirika na magonjwa kila mara.

Kaunti zingine ambako mpango huo ulitekelezwa kwa njia ya majaribio ni; Kisumu, Isiolo na Machakos.

Wagonjwa wanaougua maradhi sugu kama vile; maradhi ya moyo, kisukari, kansa kati ya mengine hulazimishwa kununua dawa nje ya hospitali.

Wakati mwingi, wagonjwa hulalamikia uhaba wa dawa na bidhaa nyinginezo muhimu.

Hata hivyo, idara ya afya iliambia kamati ya PAC kwamba orodha iliyotolewa ya dawa ambazo muda wake wa matumizi umepita, ilikuwa ni ya miaka mingi ya nyuma kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa utawala wa ugatuzi.

Walisema wakati huo kuwa dawa zilikuwa zikitumwa kutoka makao makuu ya Wizara ya Afya bila kukadiria kiwango cha matumizi yazo.

You can share this post!

Raila mbioni kurai jamii ya Abagusii kukubali BBI

Dereva anaswa kwa kukiuka sheria za usafirishaji viazi

adminleo