• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Polisi wahudumia mshukiwa wa ugaidi baada ya kumpiga risasi

Polisi wahudumia mshukiwa wa ugaidi baada ya kumpiga risasi

Na WACHIRA MWANGI

WAKAZI wa mtaa wa Tudor Mwisho, Kaunti ya Mombasa jana walistaajabishwa na jinsi polisi walivyoepuka kumuua mshukiwa wa ugaidi, wakampa huduma ya kwanza ya matibabu baada ya kumpiga risasi mguuni alipokataa kujisalimisha.

Hofu ilitanda mtaani humo ghafla alfajiri wakati polisi walipoenda kumnasa mshukiwa huyo.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo walieleza jinsi milio ya risasi ilivyotanda kwa karibu dakika 20, polisi walipowaamuru wasitoke nje wakati wa oparesheni hiyo iliyofanywa mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

Polisi hao wa kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU) hatimaye walifanikiwa kumpiga risasi mshukiwa huyo aliyetambuliwa kama Salim Aboud Khalid, 40, almaarufu kama Survivor, wakamjeruhi na kumpeleka hospitalini baada ya kumfanyia huduma ya kwanza ya matibabu.

Mkuu wa polisi wa Mombasa,Bw Eliud Monari alisema maisha ya mshukiwa hayamo hatarini kufuatia jeraha lake la risasi.

Mshukiwa alipigwa risasi mguuni akiwa mafichoni na inadaiwa alijaribu kuwashambulia maafisa wa ATPU waliomtaka ajisalimishe.

Watu walioshuhudia kisa hicho walisema kuwa maafisa wa ATPU wasiopungua 17 waliwasili katika eneo hilo wakiwa wameabiri magari matatu.

“Lengo lao halikuwa kuua. Hii ni kwa sababu mtu mmoja alipojaribu kutoroka nilisikia mmoja wao akiwaambia wenzake: ‘piga mguu’,” akasema shahidi aliyeomba jina lake libanwe.

Maafisa wa polisi walijigawa katika makundi matatu wakati wa oparesheni hiyo. Bw Monari alithibitisha kwamba mshukiwa huyo ambaye sasa yuko chini ya ulinzi mkali hospitalini ndiye alikuwa akisakwa na maafisa wa ATPU.

“Polisi walisikika wakimsihi mshukiwa aliyepigwa risasi kujisalimisha wakisema kwa sauti: ‘inua mikono juu tutakuua weeeee’,” akasema mkazi aliyeshuhudia tukio hilo.

Katika hali ambayo wakazi wengi waliona si ya kawaida, maafisa wa polisi walimpa mshukiwa huyo huduma ya kwanza ya matibabu kabla kumkimbiza hospitalini.

“Tunashukuru Mungu tumemkamata akiwa hai,” maafisa hao walisikika wakisema.

Haikubainika ni lini mshukiwa huyo atafikishwa kortini wala mashtaka yatakayomkabili.

Hata hivyo, duru zilisema wakati mwingi polisi wakiamua kutomuua mshukiwa wa aina yoyote ya uhalifu hata anapokataa kujisalimisha na kuwashambulia, huwa inamaanisha kuna habari muhimu wanazohitaji kutoka kwake.

You can share this post!

Jubilee kukosa pesa za matumizi

Gavana ataka kaunti ziwe na uhuru wa kununua dawa zao

adminleo