• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Muungano mpya wanukia Mudavadi akinyemelea Ruto

Muungano mpya wanukia Mudavadi akinyemelea Ruto

TOM MATOKE na WYCLIFF KIPSANG’

VIONGOZI wa eneo la Magharibi wameelezea uwezekano wa muungano wa kisiasa kati ya mwanzilishi wa muungano wa NASA Musalia Mudavadi na Naibu Rais Wiliam Ruto.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale alisema mikutano imekuwa ikiendelea kati ya viongozi wa Rift Valley na Magharibi kutafuta uwezekano wa wawili hao kushirikiana kutafuta uongozi wa nchi.

Akizungumza kwenye mkutano katika Kaunti ya Nandi uliohudhuriwa na Bw Mudavadi na viongozi wa eneo hilo, Bw Khalwale alisema wanalenga kuwarai Bw Ruto na Bw Mudavadi kuungana ili kutwaa urais kwenye uchaguzi wa 2022.

Viongozi wanaoendeleza mpango huo wanashikilia kwamba wawili hao wanapaswa kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kubuni muungano huo.

Juhudi hizo zilijitokeza wazi wikendi iliyopita kwenye mkutano katika Kaunti ya Nandi ambapo waliohutubu walisema familia za Kenyatta, Moi na Odinga hazipaswi kuendelea kuthibiti siasa za Kenya baada ya kipindi cha Rais Uhuru Kenyatta kukamilika.

“Baada ya miaka 50 ya uhuru, Wakenya lazima wasimame kidete ili kumaliza uongozi wa familia za Kenyatta, Odinga na Moi,” akasema Bw Khalwale.

Viongozi hao walidai kuna njama ya kumshinikiza kinara wa NASA Raila Odinga kumuunga mkono Seneta Gideon Moi wa Baringo kuwania urais 2022, hivyo kumharibia Bw Ruto nafasi ya kuwania urais.

Walisema watakataa njama hiyo na badala yake kuhakikisha jamii za Rift Valley na Magharibi zimebuni muungano.

Kwa upande wake, Bw Mudavadi alisema vyama vyote katika eneo la Magharibi vinalenga kubuni muungano wa kisiasa utakaohakikisha wana uwezo wa kubuni kushirikiana na jamii zingine nchini.

 

Kura nyingi

“Eneo hili lina kura nyingi, ila tumekuwa tukiyumbishwa kisiasa kwa muda mrefu. Wakati huo umeisha,” akasema Bw Mudavadi.

Alisema kuwa ameamua kufanya kazi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na viongozi wote wa kisiasa kutoka eneo hilo.

Pia alikosoa mazungumzo kati ya Rais Kenyatta na Bw Wetang’ula, akisema yaliwatenga viongozi wengine na hivyo yanakosa kutoa taswira ya umoja wa kitaifa.

Wakizungumza kwenye hafla hiyo Gavana wa Nandi Stephen Sang’, Seneta Samson Cherergey na Spika wa Bunge la kaunti hiyo Joshua Kiptoo walisema viongozi wa Bonde la Ufa wamekubaliana kwa pamoja kumuunga mkono Bw Ruto kuwania urais ifikapo 2022.

Bw Sang alisema kuwa viongozi kutoka maeneo ya Magharibi na Rift Valley wanapaswa kufanya kazi pamoja kwani Bw Odinga na Rais Kenyatta hawatakuwa na usemi wa atakayeiongoza Kenya baada ya 2022.

You can share this post!

Moi amtaka Ruto kukomesha siasa za 2022

Nyanya auawa kwa kushukiwa kutumia uchawi kuua watu 4

adminleo