• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Miguna alizuiliwa ndani ya choo JKIA, wasema mawakili

Miguna alizuiliwa ndani ya choo JKIA, wasema mawakili

Wakili wa Dkt Miguna Miguna, Bw Nelson Havi. Picha/Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

KIZAAZAA na sarakasi zilishuhudiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Jomo Kenyatta (JKIA) tangu Jumatatu aliporejea mwanasiasa Miguna Miguna.

Tofauti na matarajio ya wengi kuwa Bw Miguna angerejea bila kuhangaishwa, amekumbana na masaibu tele uwanjani JKIA.

Jumanne, mawakikili wake walidai kuwa alikuwa akizuiliwa chooni baada ya kukataa kusafirishwa kwa nguvu kuelekea mjini Dubai.

Dkt Miguna alilazimishwa kuingia ndani ya ndege ya Emirates na maafisa wa polisi. Lakini alisababisha ndege kuchelewa kuondoka kwa saa kadhaa alipokataa kusafirishwa na akashuka kwa nguvu.

“Miguna Miguna kwa sasa amezuiliwa ndani ya choo katika eneo la kutua ndege la Terminal 2-Arrivals na amezuiliwa kukutana na mawakili wake,” akasema Bw Nelson Havi mmoja wa mawakili wake.

Zaidi ya maafisa 100 wa polisi walitumwa uwanjani JKIA kuimarisha usalama wakati wa kurejea kwa Bw Miguna.

Kulingana na mawakili wake, Dkt Miguna alikataa kujaza fomu za kuomba uraia wa Kenya alizopatiwa na maafisa wa Idara ya Uhamiaji.

Wakili Cliff Ombetta jana alisema kwamba mteja wake hataomba upya uraia wa Kenya kwa sababu kufanya hivyo ni sawa kukubaliana na serikali kwamba si Mkenya.

Aliitaka serikali kuheshimu agizo la Mahakama Kuu ambalo iliagiza arudi Kenya baada ya kupelekwa Canada.

Ilipofika mchana, mawakili wa Bw Miguna wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo walitimuliwa na polisi kutoka katika eneo la kungojea.

Wanahabari pia hawakusazwa katika kizaazaa hicho kwani baadhi yao walishambuliwa kinyama na maafisa wa polisi.

Polisi ambao hawakuvalia sare rasmi waliwashambulia wanahabari Robert Gichira wa NTV, Stephen Letoo wa runinga ya Citizen TV na Sophia Wanuna wa KTN.

Gichira alipigwa mkono na kuvuja damu huku Bw Letoo akishambuliwa tumboni.

Bi Wanuna alipigwa kofi na mmoja wa maafisa wa polisi alipokuwa akipeperusha matangazo moja kwa moja kutoka JKIA.

You can share this post!

Miguna ni tisho kwa utawala wa Uhuru – Wadadisi

Jaji Kihara na Haji waidhinishwa na kamati ya bunge

adminleo