• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wafanyakazi wakerwa na KPA kuuza nyumba

Wafanyakazi wakerwa na KPA kuuza nyumba

Na KNA na MWANDISHI WETU

WAFANYAKAZI wa Halmashauri ya Bandari Kenya (KPA) wamekashifu vikali hatua ya usimamizi wa halmashauri hiyo ya kuuza nyumba ambazo wamekuwa wakiishi kwa zaidi ya miongo miwili.

KPA ilitangaza kuwa itauza nyumba hizo kwa bei ya Sh74milioni hatua ambayo wafanyakazi wanapinga wakisema wanapaswa kupatiwa nafasi ya kwanza kuzimiliki.

Aidha walisema kuna kesi kortini na KPA haifai kuuza nyumba hizo.

Wafanyakazi hao walisema kuwa motisha yao itapungua kwani watakosa msukumo wa kufanya kazi.

Wakizungumza Jumamosi jijini Mombasa, wafanyakazi hao walisema kuwa KPA imekiuka agizo la mahakama, kuizuia kutekeleza mpango huo.

Bw Moses Mugambi, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi hao, alisema kuwa wamekuwa wakichanga fedha kila mwezi, ili hatimaye wamiliki nyumba hizo watakapostaafu.

Bw Mugambi alishangaa kwa sababu suala hilo halikujadiliwa kwenye mkutano maalum au katika mkutano wa kila mwaka wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa walishangaa kusoma kuhusu mpango huo wa kuuza nyumba kwenye vyombo vya habari.

“Tulisoma habari za kuuzwa kwa nyumba hizo kwenye magazeti na tukashangaa kwa sababu kuna kesi kortini,” alisema na kuongeza kuwa wanahujumiwa.

Kuhusisha

Alisema kuwa halmashauri inapaswa kuwahusisha ikizingatiwa kuwa pande hizo mbili zinamiliki nyumba hiyo.

“Rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa watu maskini wanapaswa kuwezeshwa kupata nyumba wanakofanya kazi kwani hawana ardhi yao binafsi,” akasema.

Alieleza walivyoenda mahakamani mnamo 2009, ambapo mahakama iliagiza kuwa hawapaswi kuhamishwa hadi kesi hiyo itakapokamilika kusikilizwa na kuamuliwa.

Alisema kuwa walishangaa wakati walipewa barua kwamba wanapaswa kuhama kutoka nyumba hizo kufikia Oktoba 10.

Alisema kuwa walisoma kwenye vyombo vya habari kwamba nyumba hizo zitauzwa kwa Sh74 milioni kinyume na Sh14 milioni, kama ilivyokubaliwa awali.

Bw Mugambi aliomba Idara ya Uchunguzi wa Mashtaka ya Jinai (DCI) na Idara ya Masuala ya Ardhi na Ujenzi kuingilia kati ili kuhakikisha wamepata haki.

Wafanyakazi hao walisema kuwa watafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa ndio watakuwa wa kwanza kunufaika ikiwa nyumba hizo zitauzwa.

Walisema kuwa kuna njama inayoendeshwa na watu matajiri kuwanyang’anya nyumba hizo, licha ya kuzilipia kwa miaka mingi.

Bi Beatrice Mwanjala ambaye pia ni mfanyakazi na miongoni mwa wale watakaoathiriwa, alisema kuwa halmashauri hiyo inapanga kuuza nyumba zaidi ya 200 katika maeneo ya Kizingo, Mbaraki na Nyali.

Alisema kuwa wamekaa katika nyumba hizo kwa zaidi ya miaka 40, hivyo hawawezi kuhama bila taratibu zifaazo kuzingatiwa.

Wafanyakazi hao, ambao walikuwa wameandamana na familia zao, walisema kuwa zaidi ya familia 400 zitaathiriwa ikiwa mpango huo utatekelezwa.

Kulingana na wafanyakazi hao, serikali inapaswa kuingilia kati ya kusitisha mpango wa KPA wakisema wanashuku kuna watu matajiri wanaotaka kumiliki nyumba hizo.

You can share this post!

Wakazi wa Murera hatarini baada ya kuharibika mfumo wa...

Madiwani wa Mandera watoa ahadi kupitisha ‘Punguza...

adminleo