Mtoto aliyejitwika jukumu la kumlea mamaye mlemavu
NA PETER MBURU
HALI ya ulemavu kwa mama mmoja kutoka mtaa wa Shabaab, Nakuru aliyetelekezwa na familia yake miaka 18 iliyopita imemsukumia mwanawe wa kiume wa miaka kumi kuchukua majukumu mazito ya ulezi na kikazi, ambayo yanaathiri maisha na elimu yake.
Kevin Momanyi, 10 ni mwanawe Bi Irene Monari, 32, ambaye ni kiwete baada ya kupooza miguu alipokuwa na miaka minne, alipougua Polio.
Hata hivyo, Bi Monari aliteswa na kutelekezwa na familia baada ya wazazi wake kuaga na kujipata akiishi maisha yaliyojaa matatizo.
Kutokana na hali yake, Bi Monari hawezi kulipa kodi ya nyumba. Mmiliki wa ploti, hata hivyo, alimhurumia na kumruhusu kuishi pasi kulipa kodi lakini kumtaka awe akifanya usafi eneo la ploti badala yake.
“Niliiona kama bahati kwani nimeishi maisha ya kufukuzwa kila ninapoishi punde tu ninaposhindwa kulipa. Hata hivyo siwezi kufanya usafi na hivyo ni mwanangu anayefanya kazi hiyo kwa niaba yangu ili tuendelee kuishi humu,” akasema Bi Monari.
Kutokana na hayo, mama na mtoto huamka mwendo wa saa kumi na nusu alfajiri, anaosha vyombo kabla ya kumpa mamake vyombo vya kupikia chai akiwa kitandani, kisha anatoka kuanza kazi za usafi wa ploti.
Ni kazi anayofanya takriban saa moja kutokana na ukubwa wa eneo la kusafishwa, kisha baadaye anarejea na kuwaamsha ndugu zake, kuwaosha kisha kuwapa kiamsha kinywa.
Kufikia sa kumi na mbili asubuhi, mtoto huyu anachukua gari la kumsukuma mamake ‘wheelchair’ na kuanza safari ya kumpeleka katika eneo lake la kazi.
“Nina biashara ndogo ambayo niliweka baada ya kupata msaada kutoka kwa marafiki ambayo iko umbali wa karibu kilomita moja kutoka tunapoishi. Kila siku ni lazima Kevin anisukume hadi huko kabla ya kuchukua safari ya kwenda shuleni,” akasema Bi Monari.
Ukutanapo nao njiani, utakachoona tu ni mtoto aliyemakinika kumsukuma mama kwenye ‘wheelchair’, akikaza kupigana na muda ili asichelewe shuleni. Ni mchache wa mazungumzo, lakini mengi ameyazika moyoni.
“Huwa tunafika kwenye eneo la kazi takriban saa mbili ama ikiwa imepitisha dakika kadhaa na hapo Kevin anafungua mlango, anatoa kiti kidogo nje na kunishusha kwani gari hili haliwezi kutoshea ndani, kabla ya kunivuta hadi ndani,” akasema mama huyo.
Ni baada ya hapo apatapo uhuru wa kwenda shuleni, mara nyingi akichelewa kuhudhuria somo la kwanza ama kufika likiwa karibu kuisha.
Hana raha
Walimu nao walishakubali na kukumbatia maisha ya mtoto huyo, ambaye walimtaja kuwa “ameathiriwa pakubwa na maisha anayopitia, kwani hana ucheshi wala mchezo wa utoto tena na ni mnyamavu kupita kiasi,” akasema mwalimu mkuu wa Bridge International Bw Dennis Seke.
“Nilipofika miaka miwili iliyopita nilivutwa na hali ya mtoto huyo kuchelewa kupita kiasi, kukosa kuburudika pamoja na wenzake, kisha nikafahamu kuwa hata wakati wa kula chamcha alikuwa akinywa maji,” akasema Bw Seke.
Kulingana na mwalimu huyo, mtoto huyo ana uwezo wa kufanya vyema masomoni lakini maisha anayopitia yanamwathiri kwa kumpitishia katika hali ya kufanya kazi za utu uzima.
Lakini maafisa wa kushughulikia watoto Nakuru walisema kuwa hawakuwa na ufahamu wa maisha ya mtoto huyo, japo wakakiri kuwa hali ya ugumu wa maisha apitiayo mtoto huyo, polepole inalemaza elimu na mustakabali wake maishani.