Habari Mseto

Elachi ajitenga na Mariga

September 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

IDADI ya viongozi wa Jubilee wanaojitenga na mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Kibra McDonald Mariga inaendelea kuongezeka kila siku.

Wa hivi punde kumwambaa mwanasoka huyo wa zamani ni Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi.

Akiongea kwenye kipindi cha ‘Day Break’ katika runinga ya Citizen, mwanasiasa huyo wa Jubilee ametangaza kuwa atamuunga mkono mgombea wa ODM Benard Imran Okoth kwa sababu ndiye anaweza kuendeleza kazi iliyoanzishwa na marehemu Ken Okoth.

“Anayejitokeza kugombea kiti cha ubunge cha Kibra sharti awe mtu ambaye anaweza kuendeleza rekodi nzuri ya utendakazi wa marehemu aliyekuwa mbunge wa eneo hilo. Mariga hawezi kwa sababu ni mtu ambaye ‘hajawahi kupiga kura maishani mwake’,” Bi Elachi akasema.

Kulingana na Spika huyo aliyesimamishwa kazi mwaka 2018, Mariga hana tajriba ya kisiasa na kiuongozi kuongoza Kibra.

“Isitoshe, Mariga amevamia eneobunge la Kibra kutaka achaguliwe ilhali hana ufahamu kuhusu mahitaji ya wakazi,” Bi Elachi akasema.

Bi Elachi ambaye alihudumu kama Seneta Maalum katika Bunge la 10 amemshauri Bw Mariga kujizatiti kuelewa mahitaji ya wakazi wa Kibra kwanza kabla ya kutafuta nafasi ya kuwaongoza kama Mbunge.

Miradi

Amemtaka Bw Mariga kutaja miradi ya maendeleo ambayo amewahi kuanzisha katika eneobunge hilo kuwasaidia wakazi kujinasua kutoka kwa umaskini.

“Licha ya kupata nafasi ya kucheza soka ya kulipwa ng’ambo, ambapo alikuwa akilipwa mamilioni ya fedha, hajafikiria kuanzisha miradi ya kukuza talanta katika eneobunge la Kibra. Kwa hivyo, huyu sio mtu anayefaa kuchukua nafasi ya marehemu Okoth,” Bi Elachi akasema.

Viongozi wengine wa Jubilee ambao wametangaza kumuunga Bw Imran ni Mbunge Maalum Maina Kamanda, Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.