• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
Kanu yamsamehe mbunge anayempigia debe Ruto

Kanu yamsamehe mbunge anayempigia debe Ruto

BARNABAS BII na STANLEY KIMUGE

CHAMA cha Kanu hakitamwadhibu Mbunge wa Emurua-Dikirr, Bw Johana Ng’eno licha ya kuenda kinyume na msimamo wa chama hicho, kwa kumpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwa rais mwaka wa 2022.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Nick Salat Jumatano alisema chama hicho hakitaharibu rasilimali zake chache kumwadhibu mbunge huyo.

“Tulijiweka hatarini tulipomkubali kwani tulifahamu hawezi kuaminika kuwa mwaminifu kwa chama. Hata wale anaodai kuwatumikia wanajua hawezi kutegemewa. Tukimwadhibu tutakuwa tunaharibu rasilimali zetu chache,” akasema.

Huku Dkt Ruto akiwa ameonyesha wazi nia yake kuwania urais 2022, kuna dalili kwamba Mwenyekiti wa Kanu aliye pia Seneta wa Baringo, Bw Gideon Moi pia atawania wadhifa huo ingawa hajatangaza hadharani.

Seneta huyo alitawazwa kuwa mzee wa jamii ya Wakalenjin majuzi katika eneo la Mt Elgon lakini akazomwa na wandani wa Naibu Rais walioona jambo hilo kama njia ya kumhangaisha Dkt Ruto katika eneo hilo.

Mnamo Jumapili wakati wa harambee katika eneo la Kapseret, Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Ng’eno alisema hahitaji kuomba ruhusa kutoka kwa mtu yeyote ikiwemo Chama cha Kanu kabla amuunge mkono Dkt Ruto kwa urais 2022.

“Sihitaji ruhusa kutoka kwa mtu yeyote kumuunga mkono Dkt Ruto kwa urais. Nilijiunga na Kanu kwa hiari yangu mwenyewe na niko huru kufanya maamuzi kuhusu ninayetaka kumuunga mkono kwa urais,” akasema Bw Ng’eno.

Awali mbunge huyo alikuwa mkosoaji mkubwa wa Naibu Rais katika eneo la Rift Valley.

Wakati mmoja, aliungana na viongozi waasi wa Jubilee kama vile Mbunge wa Nandi, Bw Alfred Keter na Mbunge wa Moiben, Bw Sila Tiren kumshambulia Dkt Ruto.

Kinaya ni kwamba wakati mwingine, aliwapa wabunge waasi wa Jubilee changamoto kujiuzulu na kurudi debeni.

Hatua yake kujiunga na wanaompigia debe Dkt Ruto imemfaa Naibu Rais anayekumbwa na pingamizi kutoka kwa Kanu kudhibiti uongozi wa kisiasa Rift Valley.

Hata hivyo, Kanu ilipigwa jeki wakati aliyekuwa waziri Musa Sirma alipohama Chama cha ODM na kujiunga nacho, huku Dkt Ruto akizamia Kaunti ya Turkana ambako alimnasa Gavana Josephat Nanok ambaye alikuwa Naibu Kiongozi wa ODM.

Bw Nanok alitangaza ataunga mkono azimio la Dkt Ruto kuwania urais 2022.

Viongozi wa Rift Valley wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto wamekuwa wakizozana kuhusu mwelekeo wa kisiasa ambao jamii ya Wakalenjin inafaa kufuata katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa mwaka wa 2022.

Baadhi ya wabunge wakiongozwa na Mbunge wa Cherangany, Bw Joshua Kutuny wanataka jamii iwe huru kujiamulia nani anastahili kumrithi Rais Kenyatta lakini kuna kikundi kingine kinachosisitiza ni lazima jamii imuunge mkono Dkt Ruto.

You can share this post!

Feri: Joho aahidi kuita waokoaji wa Afrika Kusini

Wabunge watisha kutimua Munya na Kiunjuri kuhusu bonasi

adminleo