Habari MsetoSiasa

Wabunge watisha kutimua Munya na Kiunjuri kuhusu bonasi

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE 21 kutoka maeneo ya Mlima Kenya na Rift Valley wametisha kuwasilisha hoja ya kuwaondoa afisini mawaziri Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na Peter Munya (Biashara), ikiwa hawataingilia kati masaibu ya kushuka kwa malipo ya wakulima wa majani chai nchini.

Wakiongozwa na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria, viongozi hao jana walidai ni kutokana na uzembe wa mawaziri hao ambapo Mamlaka ya Ustawi wa Majani Chai Nchini (KTDA), imewalipa wakulima bei duni kiasi kwamba wengi wao wameshindwa kugharamia mahitaji yao ya kimsingi.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, walisema malipo ya majani chai yameshuka hadi Sh17 kwa kilo moja kutoka Sh60 mwaka jana hali ambayo imefanya wakulima kuzama kwenye lindi la umaskini.

“Ikiwa Peter Munya na Mwangi Kiunjuri ambao waliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta hatawaingilia kati suala hili haraka iwezekanavyo, basi tutaanzisha mchakato wa kuwaondoa afisini kupitia hoja bungeni,” akasema Bw Kuria.

Alimtaka Bw Kiunjuri kuchukua hatua kali dhidi ya wasimamizi wa KTDA ambao alidai ndio wanawapunja wakulima kwa kisingizio kwamba bei ya majani chai katika masoko ya kimataifa imeshuka.

“Ikiwa umeshindwa na kazi ya kupambana na matapeli hawa ambao wanawanyanyasa wakulima wetu hatutasita kukuondoa afisini,” Bw Kuria akatisha.

Naye Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua, alimtaka Bw Munya kuandaa mikutano na wakulima wa majani chai kutoka nchini ili asikie kilio chao badala ya “kuketi afisini Nairobi akinywa chai kwa mandazi”.

“Ikiwa bei ya majani chai katika mataifa ya Misri na Pakistan imeshuka kutokana na misukosuko ya kisiasa, Bw Munya kama waziri wa biashara anapaswa kusaka soko mbadala kwa zao hili. Hiyo ndiyo kazi yake,” akasema.

Nao wabunge Japheth Mutai (Bureti) na Caleb Kositany (Soy), walimtaka waziri Kiunjuri kufutilia mbali kampuni 11 za mawakala ambao hushirikiana na KTDA kuwapunja wakulima huku.

“Hawa mawakala ndio wanawaongezea wakulima wetu masaibu. Tunataka serikali kupitia wizara ya Kilimo iwapige marufuku kabisa kwa kubuni mamlaka mpya ya kuongoza shughuli ya uuzaji majani chai,” akasema.