• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Wanawake waitaka jamii kuhakikisha visiki dhidi yao vinaondolewa

Wanawake waitaka jamii kuhakikisha visiki dhidi yao vinaondolewa

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya wanawake kupata nafasi katika maswala mengi ya kijamii, imejadiliwa kwenye kongamano moja Maanzoni Lodge, Machakos.

Mkurugenzi wa shirika la Groots Kenya Bi Fridah Githuka alisema Alhamisi kwamba kwa muda mrefu wanawake hawajapata haki yao katika maswala mengi ya uongozi.

Mkurugenzi wa shirika la Groots Kenya Bi Fridah Githuka. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema shirika hilo linahamashisha wanawake kote nchini kuhusu haki zao.

Baadhi ya maswala muhimu wanayoangazia ni maswala ya urithi wa vipande vya ardhi kwa wanawake, uongozi, uhifadhi wa mazingira, na maswala ya maabukizi ya Virusi Vinavyosababisha Ukimwi; HIV-Aids.

Kongamano hilo liliangazia maswala ya kuhifadhi data kuhusu maswala ya ardhi na jinsi ambavyo wanawake wametengwa ikija kwa suala la urithi.

Hafla hiyo ilikuwa chini ya National Data Driven Advocacy for Gender na kufadhiliwa na shirika la Groots Kenya.

“Lengo letu kubwa ni kuwahamasisha wanawake ili wawe na ufahamu ya haki zao,” alisema Bi Githuku.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi katika mkahawa wa Maanzoni Lodge, Kaunti ya Machakos kwenye hafla ya kuwahamasisha waandishi wa habari jinsi ya kuripoti maswala yanayowahusu wanawake moja kwa moja.

Waandishi wapatao 30 kutoka kaunti tofauti walihimizwa kujihusisha pakubwa na maswala ya wanawake ambao hawajaangaziwa sana katika maswala mengi na nyanja mbalimbali.

Bi Githuka aliwahimiza kuangazia maswala ya ubakaji na matakwa ya wanawake.

Ukakamavu

Mwandishi na aliyekuwa mhariri katika kampuni ya Nation Media Group, Plc Bi Njeri Rugene aliwahimiza waandishi wa habari kuwa na ukakamavu wanaporipoti habari zao.

“Kabla hujaripoti habari kamili, ni sharti ufanye utafiti wako vyema. Sio vyema kuandika mambo yasiyo sahihi,” alisema Bi Rugene.

Alitaja kesi za unajisi na ubakaji kama nyeti na ambazo zinastahili kuandikwa kwa umakini mkubwa bila kuibua taharuki.

“Ukiwa mwandishi, sharti uwe makini unaporipoti habari yoyote. Sio vyema kuandika jambo linaloweza kuzua utata kwa familia na kwako pia kama mwandishi,” alisema Bi Rugene.

Waandishi walihimizwa kuwa mstari wa mbele kuangazia wananchi kinachoendelea katika jamii.

“Kila mwandishi anastahili kujituma na kujitokeza na habari zilizofanyiwa utafiti wa kina,” alisema Bi Rugene.

You can share this post!

SIHA NA ULIMBWENDE: Manufaa ya mafuta ya mbegu za alizeti...

ODM yamrarua Mudavadi

adminleo