• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Sitaacha kuongea na Mudavadi kwa ajili ya 2022 – Ruto

Sitaacha kuongea na Mudavadi kwa ajili ya 2022 – Ruto

Na BENSON AMADALA

NAIBU Rais William Ruto amesisitiza kuendelea kumwandama kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ili wabuni muungano kwa lengo la kushinda kinyang’anyiro cha urais 2022 licha ya pingamizi kutoka kwa Makamu huyo wa Rais wa zamani.

Akiongea wiki jana katika mikutano ya harambee katika maeneo ya Kidundu na Ivona katika Kaunti ya Vihiga, ngome ya Mudavadi, Dkt Ruto alisema hatakoma kuendelea kumwandama mwanasiasa huyo katika juhudi zake za kusaka uungwaji mkono wa watu wa eneo hilo.

Viongozi kutoka jamii ya Waluhya wanaomuunga mkono, miongoni mwao wakiwa wabunge kadha, seneta wa zamani wa Kakamega Dkt Bonny Khalwale na aliyekuwa Gavana wa Vihiga Moses Akaranga pia wameahidi kuendelea kumsihi Bw Mudavadi kumuunga mkono.

Vilevile, wanasiasa hao wameahidi Dkt Ruto kwamba watamfikia Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kumshawishi ajiunge na kambi ya Naibu Rais kuiwezesha jamii ya Waluhya kuwa na usemi katika serikali ijayo.

Akiongea katika Shule ya Upili ya Chavakali katika eneobunge la Sabatia, Dkt Ruto aliongeza kuwa atatumia uchaguzi mdogo katika eneo la bunge la Kibra mnamo Novemba 7, kuwahimiza watu wa jamii hiyo kumuunga mkono mgombeaji wa Jubilee MacDonald Mariga, ambaye ni Mluhya.

Naibu Rais alielezea matumaini kuwa Bw Mariga atatwaa kiti hicho cha ubunge kutoka ODM na akamtaka Bw Mudavadi kumuunga mkono mgombeaji huyo wa Jubilee.

“Ushindi wa Mariga utafungua milango kwangu kuunda muungano mkubwa na watu wa magharibi kwa lengo la kufanyakazi pamoja kule mbele,” Dkt Ruto akasema.

Kushawishi

Aliwaomba wakazi wa Sabatia kumsaidia kuzungumza na Mudavadi ili akubali aunge mkono Bw Mariga katika uchaguzi wa Kibra, badala ya mgombeaji wa ANC, Eliud Owalo.

“Kama jirani wenu niko hapa kuwaambia kuwa nawaandama kushoto, kulia, juu, chini na katikati. Mkipiga kona, nitaandamana nanyi hadi niwapate. Sitawaruhusu kufuata Raila (kiongozi wa ODM) tena,” akasema Dkt Ruto akirejelea Bw Mudavadi.

“Tuanze na Kibra, nataka ninyi watu wa Sabatia mnisaidie kumshawishi Mudavadi amuunge mkono Mariga kisha tunaweza kushiriki mazungumzo kuhusu mipango ya kinyang’anyiro kijacho cha urais. Sharti muwe ndani ya serikali baada ya uchaguzi mkuu wa 2022,” akaeleza.

Dkt Ruto alimsuta Bw Odinga kwa kutumia jamii ya Waluhya kwa manufaa yake ya kisiasa lakini amefeli kuwasaidia kimaendeleo.

Lakini kwa upande wake, Bw Mudavadi amekatalia mbali pendekezo la Naibu Rais akisisitiza kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi huyo wa ANC alitaja pendekezo hilo kama la mzaha na lisilo na nia njema akisema, “siwezi kushiriki uchaguzi mkuu wa 2022 kwa kushirikiana na Ruto.

“Muungano na Dkt Ruto hauwezi kushabikiwa na Wakenya kwa sababu huyo ni mwanasiasa asiyeaminika,” Bw Mudavadi akasema.

“Siwezi kuungana na Jubilee kwa sababu serikali imewakosea Wakenya kwa kuendeleza usimamizi mbaya wa uchumi kwa kukopa madeni kupita kiasi na kushindwa kukomesha ufisadi,” akasema.

You can share this post!

UFUGAJI: Mboga za kijani ni muhimu katika kuwapa kuku...

Mzozo polisi kuhusu ni kikosi kipi kinase magari ya makaa

adminleo