• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Msichana aliyetoweka shuleni Lamu hatimaye apatikana

Msichana aliyetoweka shuleni Lamu hatimaye apatikana

Na KALUME KAZUNGU

MWANAFUNZI wa kidato cha tatu aliyeripotiwa kutoweka tangu Jumamosi usiku kutoka shule yao ya wasichana ya Lamu, hatimaye amepatikana.

Mwanafunzi huyo anayetoka tarafa ya Mpeketoni, alishukiwa kutoroka shuleni Jumamosi saa nne usiku pindi umeme ulipotea.

Akithibitisha taarifa hizo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, amefichua kuwa msichana huyo alikutwa ‘amejificha’ kwa mjombake eneo la Mpeketoni.

Inadaiwa huenda pengine aliamua kukaa kwa mjambake kwa kuwaogopa wazazi wake baada ya kutoroka shuleni.

Msichana huyo alifichulia polisi kwamba alikuwa amekosana na mmoja wa walimu wake shuleni baada ya mwalimu huyo ‘kumsukumia’ kosa la kufanya udanganyifu katika mtihani.

“Alikuwa amepasi vyema masomo ya Kiingereza na Kiswahili. Ametuambia kwamba mmoja wa walimu wake alitisha kumwanika hadharani kwamba kupasi kwake kulitokana na yeye kuiba karatasi za mitihani mapema. Polisi bado wanaendeleza uchunguzi zaidi kuhusiana na kisa hicho,” akasema Bw Macharia.

Kwa upande wake, mama wa msichana, amethibitisha kupatikana kwa bintiye akiwa salama salimini.

Mzazi huyo amesema tayari wameandikisha taarifa kwa polisi kuhusiana na kupatikana kwa binti wao.

Amesema pia walifika shuleni kukutana na walimu ili kujua hatima ya mwana wao.

“Ni afueni kwamba msichana wangu amepatikana akiwa buheri wa afya. Tumefika shuleni kujadili hatima ya binti yangu. Tumearifiwa kusubiri hadi mwaka 2020 muhula wa kwanza utakapoanza. Wamesema lazima kamati ya Usimamizi wa shule (BOM) ikae kwanza, ijadili na kuafikiana iwapo binti yangu ataendelea kuwa mwanafunzi shuleni humo. Ningeomba watuonee imani na wamuache binti yangu kusomea shuleni hapo. Msichana ni kifungua mimba na ni tegemeo kwa familia yetu,” akasema mama huyo.

You can share this post!

Wawili wajeruhiwa vibaya baada ya gari kubingiria mara...

Maandamano kona zote Kenya

adminleo