Jumwa apata fursa nyingine kujitafutia ubabe Pwani
Na CHARLES LWANGA
MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amepata fursa nyingine kujitafutia ubabe wa kisiasa, baada ya Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi, Bw Jimmy Kahindi kutangaza kiti cha diwani wa Dabaso, kuwa wazi.
Spika alitangaza hilo Jumanne bungeni na kueleza kuwa atawasilisha agizo hilo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kutayarisha uchaguzi mdogo katika muda wa siku 90 zijazo.
Hii ni baada Mahakama Kuu kufutilia mbali uchaguzi wa Emanuel Changawa wa chama cha ODM.
Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kupima tena umaarufu wa chama cha ODM, siku chache baada ya kufanikiwa kuhifadhi kiti cha ubunge cha Kibra.
Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, jana alisema kuwa ODM wako tayari kwa uchaguzi mdogo.
“Chama cha ODM ndicho chama kinachopendwa na Wapwani na wanaotaka kugombea watapitia mchujo, kwa kuwa hatutaki kumfungia yeyote nje,” alisema katika mahojiano na Taifa Leo.
Ingawa Bi Jumwa hakupokea simu kujibu iwapo atapigia debe mgombeaji yeyote, mmoja wa wandani wake alisema kuwa huenda akatumia uchaguzi huo mdogo kupigia debe azma yake ya kuwania ugavana.
“Ingawaje sina hakika ikiwa atasimamisha mgombeaji, mama huyo yuko makini na kuendeleza ndoto yake ya kuwania ugavana wa kaunti ya Kilifi,” alisema mwandani huyo ambaye aliomba jina lake libanwe.
Chama cha ODM pia kilifaulu kushinda uchaguzi mdogo wa udiwani majuzi katika kaunti ya Kilifi.
Katika uchaguzi huo wa Kibra Alhamisi iliyopita, ingawaje kulikuwa na wawaniaji 24, ushindani mkubwa ulijitokeza kati ya Naibu Rais William Ruto kupitia kwa McDonald Mariga, na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga aliyekuwa akimtetea mgombea Benard Imran Okoth.
Uchaguzi mdogo wa udiwani unaonekana kutoa fursa nyingine kwa Bi Jumwa kuonyesha umahiri wake katika siasa za Pwani.
Ingawa uchaguzi mdogo wa wadi utaonekana usiokuwa na mvuto wowote, huenda Dkt Ruto akataka kutumia fursa hiyo kupitia kwa Bi Jumwa kujipangusa machozi kwa kushindwa Kibra.
Haya yanajiri wiki tatu baada ya Bi Jumwa ambaye anampigia debe Dkt Ruto kuwania urais, kushindwa katika kura za uchaguzi mdogo ya Ganda ulionyakuliwa na Bw Ruben Katana wa ODM, licha ya vurugu zilizosababisha kifo cha mjombake Bw Katana.
Bi Jumwa ameshtakiwa pamoja na Bw Geoffrey Okuto, kuhusiana na tukio hulo, ingawaje waliwachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 kila mmoja.
Wafuasi wake Bi Jumwa ambaye amedaiwa kulenga kumrithi Gavana Amason Kingi 2022, wamesema kujitosa kwake katika uchaguzi mdogo wa Dabaso, hata baada ya kushindwa Ganda, unatarajiwa kubadilisha mwelekeo wake wa kisiasa.
Hata hivyo, anatarajiwa kuwa na kibarua kigumu kwa kuwa wapinzani wake wawili wa kisiasa- Bw Baya na Waziri Msaidizi wa Ardhi, Bw Gideon Mung’aro, ambaye ni rafiki wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta na alikukuwa kinara Jubilee eneo la Pwani, wanatoka Dabaso.