#JkuatLivesMatter: Polisi waliopiga mwanachuo watemwa
MARY WANGARI Na MARY WAMBUI
POLISI wanne walionaswa kwenye video wakimpiga kinyama mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) Jumatatu wakati wa maandamano ya amani wamesimamishwa kazi.
Kulingana na taarifa kutoka kwa msemaji wa polisi, Charles Owino kwa vyombo vya habari, “maafisa wawili wanatoka Kituo cha Polisi cha Makongeni huku mmoja akitoka Kituo cha Polisi cha Juja.”
Haya yamejiri saa chache tu baada ya kisa hicho kuibua hisia kali nchini na kimataifa.
Wakenya waliojawa na ghadhabu walimtaka Waziri wa Usalama wa Nchi Fred Matiang’i na Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambia kuwachukulia hatua kwa haraka maafisa waliohusika.
Punde baada ya video hiyo iliyoonyesha maafisa wa polisi waliovalia magwanda yao wakimvamia na kumpiga kinyama mwanafunzi huyo, Allan Omondi, Dkt Matiang’i alijitosa mitandaoni na kuahidi kuwachukuliwa hatua wahusika katika muda wa saa 24.
“Nimetazama matukio ya JKUAT leo kwa wasiwasi usioelezeka. Utumiaji nguvu kwa polisi wafafanuliwa wazi katika Sheria kuhusu Polisi wa Kitaifa. Nimezungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi na sote tumekubaliana kuwa hatua kali na thabiti zitachukuliwa kwa afisa yeyote aliyetumia nguvu kupita kiasi, katika muda wa saa 24 zijazo,” aliandika Waziri Matiang’i kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Dkt Matiang’i alisema hayo akijibu kilio cha maelfu ya Wakenya waliofurika mitandaoni kulaani kisa hicho cha kinyama kilichowakumba wanafunzi wa JKUAT walipokuwa wakilalamikia ukosefu wa usalama chuoni humo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za kibindamu la Amnesty International lilijiunga na Wakenya kulaani kisa hicho.
Irungu Houghton ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo alikemea visa vya ukatili wa polisi katika maandamano akisema: “Ukatili wa polisi katika maandamano ni sharti ukome. Ni vigumu kwa Jamhuri kutofautisha wahuni wakiwa wamevalia au bila kuvalia magwanda ya polisi.
“Maafisa wanaokiuka kanuni za taaluma yao ni sharti waadhibiwe binafsi kwa kukosa nidhamu, kusimamishwa kazi na kulazimishwa kuwalipa wahasiriwa.”
Tukio hilo liligonga vichwa vya habari nchini na kimataifa baada ya polisi watatu kumpiga vibaya mwanafunzi ambaye hakuwa amejihami huku afisa mmoja akionekana akimponda kichwa kijana huyo aliyelala chini akijaribu kujikinga kwa mikono yake.
Wakenya walijitosa kweye mtandao wa kijamii wa Twitter jana ambapo kupitia heshitegi #jkuatlivesmatter na #stoppolicebrutality, walilaani vikali kisa hicho.
“Polisi wana nguvu ya kumpiga mateke mwanafunzi ambaye hana silaha lakini hawawezi kuwakamata majambazi Kasarani,” alisema Papi Chulo.
“Wahuni hao waliovalia sare ni sharti wakamatwe! Hakuna ufafanuzi wowote utaelezea ukatili huu,” Raymond Ofula alichangia.Baadhi ya Wakenya walihoji kuwa ni vitendo kama hivyo vya polisi vinavyofanya raia kutowaheshimu na kukosa imani na idara hiyo ya utekelezaji sheria nchini.
“Ni vigumu kuheshimu afisa wa polisi Mkenya. Ama ni fisadi, hana utu na ni katili na kwa jumla hafahamu chochote kuhusu wajibu wake,” alihoji Elijah Mokua.
“Hawa ndio maafisa wa polisi tunaoaminia maisha yetu? Haiwezekani. Ni sharti wafurushwe kutoka NPS na waadhibiwe,” alieleza Victor Kipng’eno.