• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Ruto ndiye suluhu tosha ya tatizo la ardhi Pwani, asema mbunge

Ruto ndiye suluhu tosha ya tatizo la ardhi Pwani, asema mbunge

Na KAZUNGU SAMUEL

MBUNGE wa Kisauni Bw Ali Mbogo Jumanne alisema ataunga mkono azimio la Ruto kuwa Rais mwaka wa 2022.

Akiongea katika kijiji cha Junda baada ya kutoa ripoti ya thamani ya mashamba katika eneo hilo, alisema kuwa lengo la Bw Ruto ni kuhakikisha kwamba shida za Pwani kuhusu ardhi zinapata suluhisho.

“Mtu kama huyu ni lazima tumuangalie kwa sababu alisema kuwa yuko tayari kutusaidia kupata mashamba yetu Pwani,” akasema mbunge huyo wa chama cha Wiper.

Aliwaambia wakazi kwamba Bw Ruto ndiye aliyeidhinisha wao kupatiwa ripoti hiyo wiki iliyopita, alipokutana naye kwa mazungumzo katika afisi yake Nairobi.

Ripoti hii ilikaa katika wizara ya ardhi jijini Nairobi tangu mwaka wa 2016 kwa sababu wakazi hawakuwa na uwezo wa kulipa gharama ya Sh1.7 milioni ambayo ilikuwa ikihitajika.

“Lakini juzi nilipokuwa katika afisi yake naibu huyo wa Rais alilipa Sh850,000 na kisha mara hiyo akasema ripoti iletwe mara moja.

Je, mtu kama huyu ambaye ameonyesha wazi maendeleo unaweza kumsahau kweli,” akasema.Matamshi ya Bw Mbogo yamemfanya mjumbe huyo kuwa wa pili kusema hadharani kwamba atampigia debe Bw Ruto kuwa Rais mwaka wa 2022.

Wa kwanza kutangaza waziwazi kwamba atamuunga mkono Bw Ruto alikuwa ni mbunge wa Malindi Bi Aisha Jumwa ambaye alisema hayo akiwa Voi wakati alipokuwa ameandamana na Bw Ruto katika ziara ya Pwani.

You can share this post!

Viongozi wajuta kumuunga mkono Raila uchaguzini

Tamasha zang’oa nanga kwa shairi la kusisimua

adminleo