• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
AFLATOXIN: Amri wauzaji waondoe unga hatari madukani

AFLATOXIN: Amri wauzaji waondoe unga hatari madukani

Na PIUS MAUNDU

SERIKALI ya Kaunti ya Makueni imechukua hatua kuzuia wakazi kula vyakula vilivyopikwa kwa unga wa mahindi zilizopigwa marufuku kwa madai yana kiwango kikubwa cha sumu ya aflatoxin.

Waziri wa Afya katika Kaunti, Dkt Andrew Mulwa jana aliagiza maafisa wa afya eneo hilo kuonya wakazi dhidi ya kula vyakula vilivyopikwa kwa unga wa Dola, Jembe, Kifaru, 210 na Starehe.

Bidhaa hizo ziliorodheshwa na Idara ya Ubora wa Bidhaa (KEBS) iliyosema zina kiwango kikubwa cha aflatoxin.Dkt Mulwa aliagiza wafanyabiashara wanaouza unga wa mahindi waondoe bidhaa hizo madukani mwao kama ilivyoagizwa na KEBS.

Aliagiza makampuni yaliyosambaza bidhaa hizo waende kuzichukua kabla siku saba zikamilike.Zaidi ya hayo alitaka maafisa wa afya katika kaunti wafanye uchunguzi wa kina katika kila duka kuhakikisha hakuna aina yoyote ya unga uliopigwa marufuku unauzwa.

‘Watakaokiuka maagizo haya wanafaa kuadhibiwa kwa msingi wa sheria ya vyakula, dawa na kemikali,’ akasema kwenye barua kwa maafisa wa afya ya umma.Barua hiyo ilitumwa pia kwa kamishna wa kaunti, Bw Mohammed Maalim, mkuu wa polisi katika kaunti, Bw Joseph Napeiyan, maafisa wa utawala wa serikali kuu katika kaunti, na vyama vya wafanyabiashara wa kaunti.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulionyesha kwamba kuna maduka na mikahawa ambayo bado inatumia unga uliohitajika kuondolewa sokoni.Mwenye duka mjini Makindu, aliambia wanahabari bado anahitaji kumaliza bidhaa alizonunua.

Habari ya kiupekuzi iliyopeperushwa katika Runinga ya NTV hivi majuzi ilionyesha kwamba Kaunti ya Makueni ni miongoni mwa maeneo ya Kenya yaliyoathirika zaidi kwa ulaji wa unga wa mahindi uliojaa sumu ya aflatoxin.

You can share this post!

#JkuatLivesMatter: Majina ya polisi katili yatolewa

Mjane wa Cohen aomba korti imruhusu atwae vya kwake

adminleo