• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Kuongezwa kwa riba kulivyoimarisha thamani ya shilingi ya Kenya

Kuongezwa kwa riba kulivyoimarisha thamani ya shilingi ya Kenya

Na CHARLES WASONGA

KUONDOLEWA wa sheria ya udhibiti wa riba inayotozwa na benki kwa mikopo ni mojawapo ya sababu zilizochangia kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni, hasa dola ya Amerika, wataalamu wamesema.

Hali hiyo pia imechangiwa na ongezeko la fedha zitazotumwa nchini na Wakenya wanaoishi ng’ambo haswa nchini Amerika ambako kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua.

“Katika siku chache zilizopita wawekezaji kutoka ng’ambo wamekuwa wakipata faida kutokana na kuondolewa kwa sheria ya udhibiti wa riba za benki,” Michael Mwakio anayeendesha biashara ya uuzaji hisa katika Benki ya Uwekezaji ya Sutra ameambia shirika la habari la Reuters.

Wiki jana, wabunge walishindwa kubatilisha pendekezo la rais Uhuru Kenyatta kwamba sehemu ya 33 (2) (b) ya sheria za benki iondolewe ili benki ziweze kutoza riba zinavyotaka, na kulingana na hitaji la soko la kifedha. Ni wabunge 161 pekee walikuwepo bunge wakati huo, ilhali Katiba inasema ni wabunge 233 wanaohitaji kutupulia mbali pendekezo la raia kwa mswada wowote uliopitishwa bungeni.

Kufikia Jumatano jioni dola ya Amerika ilibadilishwa kwa Sh102.05 ikilinganishwa na Sh102.25 mnamo Jumanne jioni. Thamani ya Shilingi ya Kenya dhidi ya dola moja ilitimia kiwango hiki (cha Sh102.05 kwa dola moja) mnamo Julai 4 mwaka huu.

Kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya ni faraja kwa waagizaji bidhaa kutoka ng’ambo, huku kukipunguza makali ya mfumko wa bei za bidha. Biashara katika soko la hisa pia imeimarika.

“Kenya huagiza bidhaa nyingi kutoka ng’ambo na hivyo kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola ni afueni kwao, kwani kutapunguza fedha wanazohitaji kuagiza bidhaa kutoka ng’ambo.

Kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni pia kunapunguza bei ya vyakula, mashine, kawi, mbolea na bidhaa nyinginezo ambazo huagizwa kutoka ng’ambo.

Lakini kuimarika huku kwa thamani ya shilingi ni pigo kwa sekta ya utalii kwa sababuonge watalii wengi huamua kuzuru mataifa ambako gharama ya huduma ni chini, kutokana na kupungua kwa thamani ya sarafu.

Kwa upande mwingine, mapato kutokana na uuzaji wa maua, kahawa na chai yanapungua thamani ya shilingi inapoimarika, haswa, dhidi ya dola ya Amerika.

Kiwango cha fedha zinazoingizwa nchini kutoka ng’ambo pia kimeongezeka kutokana na kupunguzwa kwa viwango vya riba vinavyotozwa na benki nchini Amerika.

Hali hiyo imewawezesha Wakenya wanaoishi Amerika kupata pesa kwa gharama ya chini kwa ajili ya kutuma nyumba ziweze kutumika kufadhili miradi.

Safaru ya Kenya vile vile inatarajiwa kuendelea kuimarika kwa sababu waagiza bidhaa za kutumika katika sekta ya kawi na mawasiliano wanaagiza bidhaa chache kwa sababu msimu wa sherehe unawadia mwezi Desemba.

You can share this post!

Wabunge wa Pwani waomba waathiriwa wa mafuriko wasaidiwe

MAKALA MAALUM: Nyandarua yalemewa na visa vya mauaji na...

adminleo