• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Biashara ya makaa kwa kiasi kikubwa inaficha al-Shabaab, asema Elungata

Biashara ya makaa kwa kiasi kikubwa inaficha al-Shabaab, asema Elungata

Na KALUME KAZUNGU

MSHIRIKISHI wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata, ameamuru maafisa wa Kutunza Misitu (KFS) kuhakikisha shughuli za uchomaji makaa kwenye misitu mbalimbali zinasitishwa mara moja.

Akizungumza wakati wa ziara yake msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu juma hili, Bw Elungata alisema biashara ya makaa ni hatari, akitaja kuwa shughuli za kuchoma makaa ndizo zinazowaficha magaidi wa al-Shabaab ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi na walinda usalama kwenye baadhi ya Kaunti za Pwani, hasa Lamu.

Alisema uchomaji makaa umekithiri eneo la Pwani katika siku za hivi karibuni, hatua ambayo alisema inahatarisha mazingira.

Alisema ni marufuku kwa watu kuingia misituni kiholela na kuchoma makaa.

Bw Elungata aliwataka maafisa wa bodi zote zinazohusiana na utunzi wa mazingira, wadau mbalimbali wa kimazingira, maafisa wa serikali na wale wasiokuwa wa serikali kujitolea kikamilifu ili kupiga vita biashara mbovu ya makaa.

“Mambo ya kuchoma makaa katika misitu yetu hasa hapa Lamu imezidi sana. Sijui ni akina nani hao wanaochoma makaa lakini tunachunguza. Hatutakubali Lamu kuwa chanzo au ngome kuu ya usambazaji wa makaa yote yanayoelekea Mombasa, Nairobi na kwingineko nchini,” akasema Bw Elungata.

Alieleza kwamba uchomaji makaa ni biashara mbaya na hatari na hata ndiyo inaficha wafuasu wa makundi ya kiuhalifu na kigaidi.

“Utafikiria anachoma makaa kumbe anatupangia njama hatari. Kwa hivyo, maafisa wetu wa kutunza misitu mlioko hapa mhakikishe uchomaji wa makaa umesimamishwa,” akasema.

Kauli ya Mshirikishi huyo wa Usalama eneo la Pwani aidha imepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya viongozi wa Lamu.

Mbunge wa Lamu Mashariki, Athman Sharif amepinga marufuku hayo ya uchomaji wa makaa kwa wakazi, akidai wengi wa wale wanaoendeleza shughuli hiyo ni kwa matumizi yao ya kinyumbani na wala si kibiashara.

Bw Sharif pia aliitaka serikali kueleza kwa kina namna marufuku hiyo itakavyotekelezwa kwani huenda ikatumiwa vibaya na walinda usalama kuwahangaisha wananchi iwapo watapatikana na makaa.

Bw Sharif aidha aliishinikiza serikali kuwaruhusu wakazi hasa wale wa maeneo ya msitu wa Boni kuendeleza uchomaji wa makaa, japo kwa kiwango kidogo ili kwaweze kujikimu kimaisha.

“Sijaridhishwa na amri ya kupiga marufuku uchomaji makaa hapa Lamu. Watu wetu wengi hapa wanachoma makaa kwa matumizi yao ya kinyumbani na wala si kibiashara. Kupiga marufuku ni kuwakandamiza. Waruhusiwe kuchoma makaa,” akasema Bw Sharif.

You can share this post!

Utata na ubovu wa ukumbi wa umma Eastleigh

Green Belt wataka serikali itoe ramani kama hakikisho...

adminleo