• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Maraga amkemea Matiang’i kuita majaji ‘wakora’

Maraga amkemea Matiang’i kuita majaji ‘wakora’

Na CHARLES WASONGA

JAJI Mkuu David Maraga Alhamisi alimshambulia Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kwa madai yake kwamba “genge la majaji waovu” wametekwa na mawakili na wanaharakati kuhujumu utendakazi wa maafisa wakuu serikali.

Kwenye taarifa fupi, Jaji Maraga alisema Dkt Matiang’i alizungumzia suala lililoko katika Mahakama ya Rufaa na alipasa kuacha mahakama hiyo kulishughulikia.

“Sio kweli kwamba kuna majaji ambao wametekwa na mawakili wanaoegemea upinzani, inavyodaiwa,” Jaji Maraga aliwaambia wanahabari jiji Nairobi Alhamisi asubuhi.

“Kile wanafanya ni kutoa maagizo ya kawaida katika utendakazi wao. Huenda wakafanya makosa katika maagizo hayo. Na tunasema kwamba wakikosea kuna nafasi ya rufaa.

Na rufaa hiyo ikiwekwa, unafaa kusubiri suala hilo lishughulikiwe. Hii ndio maana sitaki kuzungumzia kauli za waziri. Toa nafasi kwa mahakama ya rufaa kushughulika nalo,” akawaambia wanahabari.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Usalama Jumanne , Dkt Matiang’i aliwakaripia majaji aliodai wanatoa maagizo yanayoaibisha serikali na kuzuia maafisa wa serikali kutekeleza majukumu yao.

“Ni kundi la majaji ambao wanapania kutuabisha machoni pa umma,” akasema Dkt Matiang’i ambaye alishikilia kuwa serikali ililaumiwa katika sakata ya Miguna Miguna bila kupewa nafasi ya kusikizwa.

Jaji Maraga alidinda kuzungumzia hatua ya Dkt Matiang’i, Inpekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Katibu wa Uhamiaji Gordon Kihalangwa kupatikana na hatia ya kudharau mahakama kwa kumfurusha Miguna, Jaji Maraga alisema kuna mianya ambayo serikali inaweza kukataa rufaa dhidi ya uamuzi huo endapo haikuridhika nayo.

“Sina habari kwamba maafisa fulani wa Idara ya Mahakama wanatekwa na upinzani, mawakili watundu au vyombo vya habari,” akakariri.

“Masuala haya hushughulikiwa na vitengo fulani vya mahakama. Tuna kitengo cha kuchunguza uamuzi na kile cha kuangalia masuala ya kikatiba.

Wakati mwingine ni majaji hao hao hushughulikia masuala hayo,” akasema huku akirejela Jaji George Odunga aliyetoa uamuzi wa Jumatano siku chache kabla ya kwenda Machakos alikohamishiwa.

Maraga alisema maamuzi ya mahakama hutolewa kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa mbele yake. Na kabla ya chaguzi za Agosti na Oktoba, 2017, mahakama zilikuwa zimetoa uamuzi dhidi ya serikali na upinzani.

“Mahakama hushughulikia masuala kama yanavyowasilishwa. Ushahidi unaowasilishwa mbele yao na uzito wayo,” akasema Bw Maraga ambaye pia ndiye Rais wa Tume ya Idara ya Mahakama (JSC).

You can share this post!

Gavana Twaha awafurusha mawaziri kuzima malalamishi

Coca-Cola yatoa Sh42 milioni kushindaniwa na Wakenya...

adminleo