Habari Mseto

Kuku ndicho chakula maarufu nchini Kenya – Ripoti

December 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

IDADI kubwa ya Wakenya hupendelea kuagiza mlo wa kuku na pizza ambavyo ni miongoni mwa vyakula vilivyojitwalia umaarufu mkubwa zaidi mtawalia nchini, ripoti mpya imesema.

Kulingana na ripoti ya Orodha ya Jumia kuhusu Vyakula 2019, iliyoangazia mikondo ya chakula katika kipindi cha miaka mitatau iliyopita, mlo wa kuku uliorodheshwa kama chakula maarufu zaidi kinachoagizwa miongoni mwa Wakenya.

Mlo wa Pizza ulichukua nafasi ya pili kwa umaarufu huku kaimati za nyama (burgers) zikiruka hadi nafasi ya tatu kutoka nafasi ya tano mnamo 2017, kulingana na ripoti hiyo.

Ripoti hiyo vilevile ilionyesha kuwa japo umaarufu wa chakula cha India umedorora, mlo huo ungali umeshikilia nafasi ya tano.

Aidha, ripoti hiyo ilionyesha kuwepo tofauti katika ladha baina ya miji mbalimbali Kenya. Huku wakazi wa Nakuru wakiibuka kupendelea chakula cha China, wenzao wa Nairobi hupendelea kuagizia mlo wa kuku, pizza na burgers nao wateja wa Mombasa wakiegemea zaidi vyakula vya kimataifa.

Mkurugenzi wa Jumia Food Kenya kuhusu Huduma zinazoagiziwa Afrika Mashariki, Shreenal Ruparelia, alisema takwimu za Jumia zilizokusanywa kwa kipindi cha miaka saba iliyopita, ziliashiria kuwa vichocheo vya ukuaji wa huduma za uagiziaji vyakula ni pamoja na kuwepo bei nafuu, uhamasishaji na uwezo wa kupatikana katika eneo fulani la kijiografia.

“Kiamsha kinywa na chamcha vinageuka kuwa maarufu zaidi huku umaarufu wa chamcha ukipanda hadi asilimia 4.6 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 3.8 mnamo 2017.

“Chamcha kiko katika asilimia 41.1 mwaka huu 2019 kutoka asilimia 36.2 mnamo 2017,” alisema Bi Ruparelia.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo Nairobi, Bi Ruparelia alisema mabadiliko hayo yalichangiwa na hali ya kuongezeka kwa vituo vya vyakula vinavyouza vyakula kwa bei ya chini hata kwa Sh300.

Kwa mujibu wa data iliyokusanywa, hata hivyo, mkurugenzi huyo alieleza kuwa maagizo ya chajio yalipungua hadi asilimia 54.2 mwaka 2019 kutoka asilimia 60 mnamo 2017.

Vyakula vinginevyo maarufu vilivyo na uwezo wa kukua zaidi ni pamoja na vyakula vya India, Uhabeshi, na Thai.