Rais wa zamani aanza kutumikia kifungo cha miaka 12 katika jela
Na AFP
RAIS wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, alianza siku yake ya kwanza kutumikia kifungo cha miaka 12 gerezani Jumapili.
Ingawa marais wengi waliowahi kuongoza Brazil wamekuwa wakikumbwa na matatizo ikiwemo kung’atuliwa mamlakani kupitia uamuzi wa bunge au mapinduzi, na kisa kimoja cha rais kujitoa uhai, Lula ni wa kwanza kuwahi kuhukumiwa kwa ufisadi na kufungwa jela.
Makao yake mapya sasa ni ya ukubwa wa futi 160 kwa mraba pekee, katika makao makuu ya idara ya polisi yaliyo Curitiba, jiji la kusini mwa nchi ambapo upelelezi kumhusu ulikuwa ukifanywa hadi alipokamatwa.
Lula alipatikana na hatia mwaka uliopita kwa kuchukua jumba la kifahari kama hongo kutoka kwa kampuni ya ujenzi, ingawa anasema hukumu yake si ya haki.
Rais huyo aliyehudumu kwa awamu mbili kuanzia mwaka wa 2003 hadi 2011, aliwasili gerezani Jumamosi jioni kwa helikopta iliyotua kwenye paa la makao makuu ya polisi Curitiba.
Wakati helikopta ilipokuwa ikitua, waandamanaji nje ya jengo hilo waliwasha fataki huku polisi wa kupambana na ghasia wakiwarushia gesi ya kutoza machozi, na kupelekea hewa kujaa moshi na milio ya vilipuzi.
Watu wanane walipata majeraha madogo katika maandamano hayo, ikiwemo mmoja ambaye alipigwa risasi ya mpira, kwa mujibu wa idara ya zimamoto.
Lula, ambaye licha ya sakata zinazomkumba anaongoza kwenye kura za maoni kuhusu uchaguzi wa urais wa Oktoba, alijaribu kufanya hukumu yake icheleweshwe kwa kuwasilisha msururu wa rufaa katika Mahakama Kuu ya Brazil mnamo Jumatano iliyopita.
Wakati hatua hiyo ilipogonga mwamba, alianza kuzozana na maafisa wa serikali katika mtaa wa Sao Bernardo do Campo anakotoka, viungani mwa Sao Paulo.
Huku akiwa amezingirwa na maelfu ya wafuasi katika jumba la chama cha wafanyakazi wa vyuma, alipuuza agizo la mahakama lililomtaka ajisalimishe Ijumaa.
Ilipofika Jumamosi, alikubali kupelekwa jela, lakini msafara wake ukazuiliwa na wafuasi wake ambao walikuwa wakiwika “usijisalimishe, baki hapa Lula!”.
Ilibidi ashuke kwenye gari akazingirwa na walinzi na kutembea hadi kwenye gari la polisi ambalo lilimpeleka katika uwanja wa ndege wa Sao Paulo, na kusafirishwa hadi Curitiba.
Hata hivyo, seli alimofungwa ina mandhari bora ikilinganishwa na zingine, ikiwemo bafu ya kibinafsi yenye maji moto na choo.