• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Msitumie mavazi yetu asili kiholela – Wazee wa Agikuyu

Msitumie mavazi yetu asili kiholela – Wazee wa Agikuyu

Na MACHARIA MWANGI

WAZEE wa jamii ya Agikuyu wameghadhabishwa na tabia ya baadhi ya wanasiasa kuvaa mavazi ya kitamaduni ya jamii hiyo kiholela.

Wazee hao wa Chama cha Utamaduni wa Gikuyu, almaarufu kama Kiama kia Ma walisema ni makosa makubwa wanasiasa kuvaa mavazi ya kitamaduni ya jamii hiyo wakati wanapofanya mikutano yao ya kisiasa.

Wakizungumza Naivasha, Kaunti ya Nakuru jana, wazee hao wakiongozwa na mwenyekiti wao wa kitaifa Ndung’u Wa Gaithuma walikashifu baadhi yao ambao, kulingana nao, ndio huruhusu wanasiasa kuvaa mavazi hayo bila kuzingatia masharti ya kitamaduni.

Alisema mavazi hayo huwa na maana yake na hustahili tu kuvaliwa na watu waliopitia matambiko ya kitamaduni.

“Tumekasirishwa na jinsi baadhi ya wanasiasa hutumia vibaya mavazi yetu ya kitamaduni wakisaidiwa na baadhi ya wenzetu ambao walitimuliwa katika mabaraza ya wazee. Mavazi hayo yana maana muhimu sana kitamaduni,” akasema.

Aliongeza: “Lazima tukomeshe tabia ambapo wanasiasa wanaruhusiwa kuvaa mavazi hayo bila idhini ya wanachama wetu halisi.”

Wanasiasa wengi wamekuwa wakionekana wakipewa mavazi na vifaa vingine vya tamaduni mbalimbali wakiwa katika harakati zao za kujipigia debe kisiasa.

Wakifanya hivyo huwa inasemekana wameidhinishwa kuwa wazee wa jamii hizo hata kama wao ni wa jamii tofauti ambazo tamaduni zao haziwiani kabisa na zile za jamii wanazosemekana kuingizwa kuwa wazee.

Mazoea

Mbali na jamii ya Wakikuyu, matukio haya yamekuwa yakishuhudiwa pia miongoni mwa jamii nyingine kama vile za Mijikenda, Waluo na jamii za Bonde la Ufa.

Lakini wakati mwingi, hatua hii husababisha mgawanyiko katika makundi ya wazee wa jamii kwani wengine hujitokeza kudai waliotoa mavazi hayo hawatambuliki kuwa wazee wa kuongoza jamii.

Afisa mwingine wa kikundi cha Kiama Kiama, Kigochi Wamiri alisema baada yao kushauriana siku nzima, wazee hao wa kitamaduni waliamua kwa pamoja kwamba watachukua hatua kukomesha tabia hiyo.

“Tutaadhibu mwanachama yeyote ambaye atakiuka mwongozo wetu ulio wazi. Wanasiasa wanaotaka kujiunga na makundi yetu ya kitamaduni wanafaa wajiandae kutimiza mahitaji yote yanayohitajika kabla waingizwe katika kikundi chetu,” akasema.

Bw Wamiri alitaka wanachama wa kundi hilo la wazee wawe wakitafuta ushauriano kwa mapana kabla kutekeleza tambiko lolote la utamaduni wa Wakikuyu.

“Katika utamaduni wetu, mavazi ya jamii ya Wakikuyu huwa hayapeanwi kama zawadi na hufaa kuvaliwa kabla saa kumi na mbili jioni. Hiyo ndiyo sheria,” akaongeza.

Wazee hao waliomba viongozi kuheshimu uongozi wa baraza lao na kufuata kikamilifu kanuni zao la sivyo waadhibiwe.

Wakati huo huo, walimkashifu mwanasiasa wa Nakuru ambaye hawakumtaja, waidai alienda kuchafulia jina wanachama wa baraza la wazee pamoja na shughuli zao.

You can share this post!

Mauzo duni Krismasi, wafanyabiashara waumia

Mama mkwe abeba chupi za jombi Krismasi

adminleo