Habari Mseto

Wezi warejesha kuku wa kasisi kwa kuhofia laana

January 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WANYORO

WAZEE wa baraza la Njuri Ncheke wamefanikiwa kurejesha kuku 24 kati ya 60 walioibwa kutoka nyumbani kwa kasisi wa Kanisa Katoliki baada ya kutishia kuwalaani wezi katika eneo la Nchiru, Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru.

Wazee hao walisema wezi walisalimisha kuku hao kwa kuhofia kupata laana inayojulikana kama ‘kithiri.

Wazee hao walikuwa wametoa makataa ya siku 21 kwa wezi hao kujisalimisha.

Laana hiyo inahusisha kiapo ambapo wahusika wanaaminika kufa wanapokataa kusalimisha mali ya wizi.

Mwenyekiti wa Njuri Ncheke wa Tigania West Julius Mung’athia walisema wazee waliingilia kati baada ya Kasisi Francis Riwa Limo kulalamika kuwa kuku wake wa kutaga mayai waliibwa.

Muda mfupi baada ya taarifa kuenea kwamba wazee hao wamefanya tambiko la kuachilia laana hiyo, wafanyabiashara wawili walisalimisha kuku kutokana na hofu kuwa wangekufa.

“Tulighadhabishwa na wezi hao kwa sababu kasisi huyu anatumia kuku hao kulisha watoto yatima anaoishi nao. Tulimwakikishia kuwa tungemsaidia kurejesha kuku hao. Tunafanya kazi kwa kushirikiana na makanisa, jamii na serikali,” akasema Mzee Mung’athia.

Alisema kuwa wazee wamesikitishwa na ongezeko la visa vya uhalifu katika eneo hilo.

Hivi karibuni watu watatu walifariki baada ya kuuawa na watu wasiojulikana.

Nguruwe wanane wa Kasisi Riwa pia waliuawa kwa kulishwa sumu wiki chache zilizopita.

Mzee Mung’athia alisema kuwa baraza la Njuri Ncheke pia lilisaidia kuvumbua kitendawili kuhusiana na wizi wa magunia 36 ya mahindi yaliyoibwa kutoka nyumbani kwa kasisi huyo.

“Mwanaume aliyeiba mahindi hayo kutoka eneo la Kamugaa aliaga dunia. Tuna hakika kwamba kuku waliosalia watarejeshwa,” akasema.