Makamishna walikubaliana nimsimamishe kazi Chiloba – Chebukati
Na VALENTINE OBARA
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, ametetea uamuzi wa kumsimamisha kazi kwa muda Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw Ezra Chiloba.
Bw Chebukati alithibitisha kwamba uamuzi huo ulitokana na uchunguzi kuhusu ununuzi wa vifaa vilivyotumiwa katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo inashukiwa kanuni hazikufuatwa kikamilifu.
Kulingana na mwenyekiti huyo, uamuzi wa kumwagiza Bw Chiloba kwenda likizo ya lazima kwa miezi mitatu ulifanywa kwa njia ya kura ya makamishna waliohudhuria mkutano huo, na wengi wao walikubaliana nao.
“Likizo hiyo ya miezi mitatu itawezesha kukamilishwa kwa uchunguzi. Ni muhimu itambuliwe kuwa kwa kuamua kufanya uchunguzi wa kina, tume inatekeleza jukumu lake la kulinda rasilimali za umma,” akasema kwenye taarifa iliyotolewa na IEBC Jumatatu usiku.
Mkutano wa makamishna ulifanywa Ijumaa iliyopita. Tume hiyo ilibaki na makamishna sita baada ya Dkt Roselyne Akombe, kujiuzulu mwaka uliopita.
Duru zilisema kamishna Margaret Mwachanya yuko ziarani katika Milki ya Kiarabu (UAE), naye Naibu Mwenyekiti Consolata Maina aliondoka mkutanoni wakati makamishna walipotofautiana kuhusu ripoti ya uchunguzi iliyowasilishwa na Bw Chebukati.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na makamishna Boya Molu na Prof Abdi Guliye ambao waliunga mkono kusimamishwa kazi kwa Bw Chiloba, na Dkt Paul Kurgat ambaye alipinga uamuzi huo.
Mbali na mamlaka ya Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Chiloba pia huwa ni katibu katika tume hiyo lakini hakuhudhuria mkutano wa Ijumaa.
Chiloba haaminiki
Mashirika ya kijamii yalisema matukio haya ni thibitisho la wazi kwamba wakati umefika kwa Bw Chiloba kujiuzulu kwani hawezi kuaminika tena kusimamia tume hiyo.
Mratibu wa Shirikisho la Mashirika ya Kijamii (CSRG), Bw Suba Churchill, alisema udhaifu wa Bw Chiloba ulianza kuonekana mwaka uliopita wakati Mahakama ya Juu ilipofutilia mbali matokeao ya uchaguzi wa urais uliofanywa Agosti 8, kwa msingi kuwa kanuni za kisheria na kikatiba hazikufuatwa katika maandalizi yake.
Alisema mashirika ya kijamii yaliwasilisha ombi wakati huo kwa IEBC na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ili maafisa wakuu wa tume hiyo wachunguzwe lakini hadi sasa hawajapewa ripoti kuhusu uchunguzi uliopendekezwa.
“Sasa inaonekana kuna watu wenye ushawishi mkubwa ambao wanashirikiana na baadhi ya makamishna wa IEBC kulinda maafisa fulani wa tume ambao wanastahili kushtakiwa kwa uhalifu,” akasema Bw Churchill.
Wito wa kumtaka Bw Chiloba ajiuzulu ulianza kutolewa mwaka uliopita na Muungano wa NASA ambao ulidai alikuwa akishirikiana na Chama cha Jubilee ili kumpendelea Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa urais.