• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
Njaa yanukia akiba ya mahindi nchini ikiisha

Njaa yanukia akiba ya mahindi nchini ikiisha

Na BARNABAS BII

KENYA inakumbwa na hatari ya kuathiriwa na baa la njaa baada ya kiwango cha zao la mahindi kupungua kwa kiwango kikubwa.

Maafisa wasema kwa sasa, Hifadhi ya Chakula cha Dharura (SFR) inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa viwanda vya kusaga unga kwa ununuzi wa zao hilo wanaonunua moja kwa moja kutoka kwa wakulima kutokana na uhaba unaojongea kufuatia mavuno duni msimu uliopita.

Mwenyekiti wa SFR, Dkt Noah Wekesa jana alithibitisha kwamba shirika hilo la kitaifa limeuza magunia yote milioni nne ya mahindi chini ya mpango wa dharura huku likipanga kununua mifuko milioni tatu kutoka kwa wakulima kwa bei nafuu.

“Kwa sasa, hatuna hifadhi yoyote ya mahindi ya dharura lakini tuna pesa za kutosha kununua zao hilo kutoka kwa wakulima au kuagizia zao hilo kutoka nje,” alidokeza Bw Wekesa.

Wamiliki viwanda vya kusaga unga wanalipa wakulima kati ya Sh3,200 na Sh3,400 kwa kila mfuko wa kilogramu 90 wa mahindi kutokana na uhaba wa nafaka hizo sokoni, hali inayowafaidi wakulima.

“Bodi ya Nafaka na Mazao Nchini inakabiliwa na kibarua kigumu huku ikinunua mahindi kutoka kwa wakulima ambapo inalazimika kununua kwa zaidi ya Sh4,000 kwa kila kilogramu 90 na kulipa papo hapo katika ushindani mkali wa kuwapiga chenga wenye viwanda na wafanyabishara wengine,” Bw Wilson Too, mkulima wa mahindi ya kuuza kutoka Moiben, kaunti ya Uasin Gishu, anasema.

NCPB ilinunua mifuko 417,000 ya mahindi miongoni mwa mifuko milioni mbili ya mahindi iliyolengwa msimu uliopita kwa Sh2,300 kwa kila mfuko wa kilogramu 90.

Lakini wataalam wa kilimo na wamiliki viwanda vya kusaga unga wameonya kuhusu uhaba wa chakula unaonukia ambao huenda ukailazimu serikali kuangazia upya uagiziaji wa mahindi huku idadi kubwa ya wakulima wa mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wakimaliza hifadhi yao kutokana na mavunoduni msimu uliopita.

Wamiliki hao wa viwanda wasema nchi inakabiliwa na uhaba wa mahindi licha ya kuagizwa kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

You can share this post!

Sonko apumua madiwani kusema hawatamng’atua

Wito Washiali ashikwe kwa kushambulia mtu

adminleo