Ibrahim Akasha ndani miaka 23
Na RICHARD MUNGUTI
HIMAYA ya uuzaji dawa za kulevya ya familia ya marehemu Ibrahim Akasha aliyeuliwa Uholanzi imeporomoka kufuatia kusukumwa jela kwa kitinda mimba wake Ibrahim Akasha miaka 23 na Mahakama ya Amerika.
Kusukumwa jela kwa Ibrahim kulitia kikomo kesi ya muda mrefu iliyokuwa inaendelea dhidi yake na nduguye Baktasha. Meneja wa biashara hiyo raia wa India Goswami Vijay mwenye umri wa miaka 59 na raia wa Pakistani Gulam Hussein wangali wanasubiri adhabu yao kupitishwa.
Punde tu baada ya Jaji Victor Marrero kumuhuku Ibrahim, wakili Dawn Cardi aliyemtetea akionyesha mshtuko alisema “ adhabu hii ni kali na haifai kamwe.”
Uamuzi ulichukua saa mbili kukamilishwa.
Bi Cardi alikuwa amemsihi Jaji Marrrero amfunge jela Ibrahim miaka 10 badala ya miaka 25 iliyofungwa kaka yake Baktasha Augosti mwakaa uliopita.
Viongozi wa mashtaka Amerika walikuwa wameomba mahakama iwasukumie kifungo ch maisha ndugu hao.
Hata ingawa majaji hawakuwatosa jela maisha ndugu, adhabu hizo ni ushindi mkubwa kwa Serikali ya Amerika katika jitihada zake za kuangamiza biashara ya uuzaji wa mihadarati.
“Ibrahim alikuwa mtu wa mkono wa Baktash,” alidokeza Bi Cardi Ijumaa , huku akisema , “ Baktash ndiye alikuwa kinara na kitovu cha biashara hiyo ya mihadarati.”
Wakili huyo alieleza mahakama Ibrahim alikuwa na umri wa miaka 10 tu baba yao alipouawa Uholanzi ndipo Baktash akatwaa usukani wa kusimamia “ biashara hiyo ya ulanguzi wa dawa.”
Bi Cardi alisimulia kuwa “ Ibrahim alikuwa kama tarishi wa Baktash.”
Wakili huyo alisema mlanguzi mwingine raia wa Pakistan, Shahbaz Khan , aliyekuwa ameapa kuingiza maelfu ya dawa za kulevya Amerika alifungwa miaka 15 tu Novemba 2019 na mahakama hiyo ya New York, Amerika.
Ibrahim na Baktash Akasha walikiri kula njama za kupeleka kilo 99 za heroin Amerika mnamo Oktoba 2018.
Alisema mteja wake (Ibrahim) alikamatwa wakati wa oparesheni iliyotekelezwa na maafisa wa usalama wa Amerika wa kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya.
Hata hivyo Ibrahim mwenye umri wa miaka hakuonyesha mshtuko hata baada ya kusikia muda atakaoishi jela.
Ibrahim aliyekuwa amefungwa pingu miguuni na mikononi na kuvalia gauni ya jela yenye rangi ya kijivu aliomba msamaha.
Alisema, “Nachukua fursa hii kuomba msamaha familia zilizoathiriwa na biashara hii ya dawa za kulevya niliyokuwa nafanya.”
Ibrahim alimsihi Jaji Marrero “amwonee huruma” ndipo arudi kujiunga na familia yake , mkewe na watoto wake watatu wanaoishi mjini Mombasa.
Lakini jambo hilo halitawezekana hadi mwaka wa 2037 atakapokamilisha kifungo na kurudishwa nchini Kenya. Amekuwa jela kwa miaka mitatu na huenda akapunguziwa kifungo iwapo ataonyesha uadilifu akiwa kifungoni.
Kiongozi wa mashtaka Jason Richman aliomba mahakama itilie maanani azma ya ndugu hawa ya kulangua kilo 99 za dawa za kulevya hadi Amerika.
Bw Richman aliomba korti itilie maanani mipango ya familia hiyo ya Akasha ya kupanua “Himaya ya Akasha” ya kusambaza biashara yao ya ulanguzi wa dawa hadi Amerika.
Kiongozi huyo alieleza korti ndugu hao walinuia kuuza kwa fujo heroin na Methamphetamine nchini Amerika.
Ndugu hao walikamatwa na maafisa wa usalama kutoka Amerika waliojifanya walanguzi wa dawa za kulevya kutoka Columbia.