Walimu wote 88,000 waajiriwe kazi ya kudumu – Sossion
Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kimeitaka serikali kuhakikisha kuwa walimu wote 88,000 watakaoajiriwa ni wale wa kudumu.
Katibu Mkuu wa chama hicho Wilson Sossion Jumatano alisema chama hicho kinapinga wazo la kuajiriwa walimu 68,000 kama vibarua huku 20,000 wakiajiriwa kwa kandarasi ya kudumu.
“Sisi kama chama tunaunga mkono mpango wa serikali wa kuajiri walimu 88,000 kama njia ya kupunguza uhaba wa walimu unaoshuhudiwa nchini. Lakini tunapinga vikali wazo la kuajiriwa kwa jumla ya walimu 68,000 kati ya hao, kama vibarua,” Bw Sossion ambaye pia ni Mbunge Maalum akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.
Alisema itakuwa ni kitendo cha ubaguzi kwa serikali kuwaajiri walimu kwa masharti tofauti ilhali wamehitimu kwa njia sawa.
“Kuna mantiki gani kuajiri walimu 20,000 kwa kandarasi ya kudumu na kuwabagua wengine 68,000 kwa kuwaajiri kama vibarua ilhali wote wamehitimu kwa njia sawa? Tunapinga ubaguzi huu japo tunafurahi kwamba angalau serikali imeamua kuanza kushughulikia tatizo la uhaba wa walimu katika shule za umma,” Bw Sossion akasema.
Katibu huyo mkuu alipendekeza kuwa mabilioni ya fedha ambayo serikali ilitenga kwa mradi wa ununuzi wa vipatakalishi yalielekezwa katika mpango wa kuwaajiri walimu.
“Sh17 bilioni ambazo kufikia sasa zimeelekezwa kwa mpango wa ununuzi wa vipakatalishi kwa watoto wa darasa la kwanza zingetumiwa kuajiri walimu. Kiasi hicho cha fedha kinaweza kuajiri walimu 40,000 kwa kandarasi ya kudumu,” akasema Bw Sossion.
TSC yapewa Sh26 bilioni
Mnamo Jumanne wabunge walipitisha Sh26 bilioni ambazo Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) iliomba kuiwezesha kuajiri walimu 88,000.
Hata hivyo, jumla ya walimu 68,00 wataajiriwa kama vibarua kwa gharama ya Sh16 bilioni huku walimu 20,000 wakiajiriwa kwa mkataba wa kudumu kwa gharama ya Sh10 bilioni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu Julius Melly alisema hatua hiyo inalenga kupunguza uhaba wa walimu nchini ambao umefikia kiwango walimu 104,821.
“Tumejitolea kuhakikisha kuwa suala hili la uhaba wa walimu linashughulikiwa mara moja,” akasema Bw Melley ambaye ni Mbunge wa Tinderet, Jumanne kamati yake ilipokutana na Afisa Mkuu wa TSC Nancy Macharia na Waziri wa Elimu Amina Mohammed.
Dkt Macharia na Bi Mohammed walikuwa wameitwa na kamati hiyo kujibu masuala kutoka kwa Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma kuhusu kero la uhaba wa walimu katika eneo bunge lake.
Walimu 104,000 wanahitajika
Macharia alisema kuna uhaba wa walimu 40,972 katika shule za msingi huku shule za upili zikikabiliwa na upungufu wa walimu 63,849.
Sera ya serikali ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) wanajiunga na shule za upili pia imeleta hitaji la walimu 50,789 zaidi kwa kipindi cha miaka minne.
“Kufikia sasa sajili ya TSC ina jumla ya walimu 291,785 ambao hawajaajiriwa licha ya kuhitimu. Idadi hii ni juu zaidi kuliko kiwango cha uhaba wa walimu katika shule za umma,” akasema.
Afisa huyo aliwahakikishia wabunge kuwa TSC itahakikisha kuwa walimu watakaoajiriwa wanasambazwa kwa njia sawa nchini.