HabariSiasa

Uhuru na Ruto, nani anamsaliti mwingine?

January 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

UHUSIANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, unaendelea kuwa baridi huku makundi mawili katika chama tawala cha Jubilee yakilaumiana kwa usaliti.

Washirika wa Dkt Ruto wanamlaumu Rais Kenyatta kwa kumsaliti na kumtenga serikalini kinyume na maafikiano yao walipounda chama cha Jubilee.

Wanahisi kwamba Dkt Ruto alimsaidia Uhuru kuwa rais lakini sasa kuna njama ya kumzuia kuwa na usemi katika chama tawala na hata serikalini.

Ingawa Dkt Ruto amekuwa akidai uhusiano wake na Rais Kenyatta uko thabiti, washirika wake wa kisiasa wamekuwa wakimlaumu Rais hadharani wakidai baadhi ya maamuzi yake yanalenga kumtenga naibu wake, mshirika wake wa kisiasa tangu 2013.

Nao washirika wa Rais Kenyatta wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto kwa kumkaidi mkubwa wake wakisema kufanya hivyo ni kusaliti kiapo cha ofisi yake.

Wanaomuunga Rais wanadai kwamba amekuwa na kiburi na huwa anatuma washirika wake kumshambulia Uhuru. Wale wanaounga Ruto wanasisitiza kuwa Rais ameagiza maafisa wa serikali kumhangaisha naibu wake.

Kulingana na washirika wa Dkt Ruto, Rais Kenyatta amesaliti naibu wake kwa kukosa kumwidhinisha kuwa mrithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na kumzima asitekeleze wajibu wowote katika kufanikisha ajenda za serikali.

Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa manifesto ya Jubilee na Ajenda Nne Kuu za serikali ndizo zinazofaa kupewa kipaumbele. Hata hivyo, Rais Kenyatta amepatia kipaumbele mchakato wa Jopokazi la Maridhiano (BBI) na vita dhidi ya ufisadi ambazo washirika wa Dkt Ruto wanahisi zinamlenga.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Kenyatta alikuwa akifahamisha wafuasi wa Jubilee kwamba atahudumu kwa miaka kumi na kisha ampishe Ruto kutawala wa miaka kumi.

“Tunasema hivi, nipeni nafasi nimalize miaka yangu kumi na Ruto afanye yake kumi,” Rais alisema kwenye mikutano ya kampeni hasa eneo la Rift Valley, ngome ya Dkt Ruto.

Hata hivyo, Rais Kenyatta amekuwa akisema ni Mungu anayejua atakayekuwa rais baada yake na kuwa chaguo la atakayemrithi litawashangaza Wakenya. Washirika wa Dkt Ruto wanahisi kwamba Rais Kenyatta amesaliti Dkt Ruto na kusahau manifesto ya Jubilee na kuungana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ili kuzima azma ya naibu wake ya kuwa rais.

Dkt Ruto mwenyewe amekuwa akimlaumu Bw Odinga kwa kuwa na njama ya kusambaratisha chama cha Jubilee na kumfanya atengwe serikalini.

“Tulipounda Jubilee tulikuwa na manifesto na mwelekeo wa kuunganisha Wakenya na kufanikisha maendeleo. Lakini tumeona usaliti wa hali ya juu katika kipindi hiki cha pili,” alisema mwandani wa Ruto aliyeomba tusitaje jina lake akisema washirika wa naibu rais wamekuwa wakidhulumiwa.

Baada ya kuapishwa kwa kipindi cha pili, Rais Kenyatta alitangaza kipindi cha siasa kilikuwa kimeisha lakini Dkt Ruto aliendelea kutembelea maeneo tofauti nchini kuendeleza siasa akidai alikuwa akizindua miradi ya maendeleo.

Katika mikutano yake kote nchini, washirika wake huwa wanaidhinisha azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wanasema kwamba Dkt Ruto alimsaidia Rais Kenyatta kushinda urais kwenye chaguzi za 2013 na 2017 akiwa na matumaini kwamba atarudisha mkono lakini kwa sasa haonekani kuwa na mipango hiyo.

Ingawa Dkt Ruto anahisi kwamba Rais Kenyatta ameacha kutekeleza manifesto ya Jubilee, wandani wa Rais wanahisi kwamba ni yeye aliyejisaliti kwa kuhujumu mkubwa wake hasa kwa kutokomesha siasa, kupinga vita dhidi ya ufisadi na kupuuza Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakidai kuwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI unalenga kumzima kisiasa.

“Ruto na wandani wake wamekuwa wakipinga miradi ambayo Uhuru anapenda sana kama BBI na kusahau kuwa ni mchakato ulioanzishwa na mkubwa wake na kwa rais na washauri wake, huu ni usaliti wa hali ya juu na kukosa heshima. Naibu Rais hafai kumpinga mkubwa wake hadharani,” alisema mdadisi wa siasa David Bosire.