Habari Mseto

Mwanamke anaswa akiuza mtoto Sh30,000

January 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na STANLEY NGOTHO

MWANAMKE katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos alikamatwa wikendi pamoja na wenzake wawili alipojaribu kumuuza mtoto wake wa siku nne kwa Sh30,000.

Kukamatwa kwake kulifanikishwa na ushirikiano wa vikosi vya usalama baada ya kufanya uchunguzi wa miezi kadhaa.Maafisa wa polisi waliweka mtego baada ya malalamishi ya umma kuhusu biashara ya uuzaji watoto, wakafanikiwa “kumnunua” mtoto wa kiume kwa Sh30,000.

Polisi waliovalia kiraia kwa msaada wa mdokezi walikuwa wakimfuata Bi Imani Wanza na Bi Ann Nzeli, 42, ambaye aliwapeleka kwa Bi Muthoki, 20 ambaye wakati huo alikuwa mjamzito.

Kulingana na mdokezi, Bi Muthoki alizaa nyumbani kwa msaada wa mkunga katika mpango uliowekwa kisiri yeyote asijue.

Baada ya mpango, huo Bi Nancy alipelekwa kwenye baa na lojingi iitwayo Makueni huku wenzake wakimtafutia mteja.

“Mama na mtoto wake walikaa chumbani kwa muda wa siku tatu kwani kiumbe aliyejuwa akimtafutia mteja hakujua polisi wanamfuata,” akaambia Taifa Leo.

Habari zaidi zinaonyesha kuwa mtoto wa kiume huuzwa pesa zaidi kuliko mtoto wa kike.Vilevile, hakuna stakabadhi zozote huwa katika biashara hii.

Mtoto huuziwa anayetoa peza nyingi kuliko wengine.Ijumaa iliyopita, maafisa wa polisi waliovalia kiraia walipelekwa kununua mtoto na broka.

Walijadiliana bei ya mtoto na wakaafikiana Sh30,000 pesa taslimu.Hapo awali walikuwa wameagizwa kuleta nguo na mipango ya awali ilifanywa kumpeleka mtoto kwa kliniki ya karibu akaguliwe kabla ya mipango kukamilika.