• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Uingereza itakoma kutoa tahadhari za usafiri Kenya – Boris Johnson

Uingereza itakoma kutoa tahadhari za usafiri Kenya – Boris Johnson

Na PSCU

WAZIRI Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amemhakikishia Rais Uhuru Kenyatta kwamba taifa hilo litaacha kutoa tahadhari za usafiri dhidi ya Kenya kwani hatua hiyo huathiri uchumi wa nchi.

Walipokutana Jumanne katika ofisi ya Waziri Mkuu iliyo katika barabara ya No.10 Downing jijini London, wawili hao walijadili madhara ya taarifa hizo ambazo mara nyingi hutolewa panapotokea shambulio la kigaidi nchini.

Rais Kenyatta alimshukuru Waziri Mkuu Johnson kwa kutambua athari za taarifa hizo za kusafiri pamoja na hakikisho la Bw Johnson kwamba taarifa hizo hazitatolewa tena dhidi ya Kenya.

“Kinachotokea baada ya kutolewa kwa taarifa hizo ni kwamba kazi zinapotea hasa katika sekta ya utalii na hivyo kuwapa nafasi vijana wengi kujitolea kwa mafundisho ya itikadi kali,” akasema Rais Kenyatta.

Walikubaliana kwamba Kenya na Uingereza sharti zishirikiane zaidi katika vita dhidi ya ugaidi.

“Tungependa kushirikiana kukabili ugaidi. Hawa wahalifu wameendelea kudhuru watu wetu na huu ni wakati mwafaka wa kushirikisha juhudi zetu kuwakabili,” akasema Rais.

Bw Johnson alisema anatambua kwamba Kenya imeathirika sana kutokana na ugaidi na hivyo kuna haja ya kushirikisha juhudi kuukabili uovu huo.

Alisema kambi ya Uingereza ya mafunzo ya kijeshi iliyo Nanyuki itaendelea kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Kenya kama njia ya kuimarsiha ushirikiano kati ya mataifa haya mawili.

Kando na hayo, walijadili jinsi biashara itakavyokuwa baada ya Uingereza kujiondoa katika Muungano wa Ulaya.

Rais alikuwa ameandamana na Mawaziri Ukur Yatani, Monica Juma na Adan Mohammed pamoja na Balozi wa Kenya nchini Uingereza Manoah Esipisu.

Kuhusu mpango wa kulikarabati Jiji kuu la Nairobi, Rais Kenyatta alisema Kenya iko makini kuhakikisha hadhi ya jiji hilo lililotambulika kama “city in the sun” inarejeshwa.

“Mpango wa ukarabati unaendelea lakini mbali na hilo tunatafuta suluhisho la uchukuzi bora wa watu wetu. Hii ni nyanja ambayo tunaweza kushirikiana,” akasema Rais Kenyatta.

Alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutoa hakikisho kwamba Uingereza iko makini kushirikiana na Kenya katika kusuluhisha mipango ya miji na uchukuzi.

Pia, viongozi hao wawili walikubaliana kushirikisha juhudi za kutoa makaazi ya gharama nafuu nchini Kenya ambayo ni mojawapo wa nguzo nne za ajenda kuu ya maendeleo.

Akitoa mfano wa baadhi ya mitaa ya zamani iliyojengwa katika eneo la mashariki la Jiji kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza, Rais Kenyatta alisema kujihusisha kwa Uingereza katika harakati za kutoa makaazi ya gharama nafuu hapa nchini kutahakikisha ufanisi wa mpango huo.

Kuhusu biashara, Bw Johnson alisema Uingereza inatambua Kenya kuwa mshirika muhimu barani Afrika.

Alisema biashara kati ya mataifa haya mawili imeimarika kwa miaka mingi lakini bado kuna nafasi ya upanuzi zaidi akigusia ongezeko la hitaji la bidhaa za Kenya kama vile majani chai.

Vile vile walijadili ushirikiano kati ya mataifa haya mawili kuekeza katika teknolojia ya kusaidia kuhifadhi mazingira, nyanja ambayo Uingereza imepiga hatua kubwa.

Bw Johnson alisema Uingereza iko makini zaidi kuisaidia Kenya kuafikia asilimia 100 ya vianzo vya kawi safi.

You can share this post!

Uhuru kuenda Ufaransa kusaka wawekezaji

Njonjo aadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa

adminleo