Habari Mseto

UoN: Pigo kwa Magoha

January 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

PROFESA Stephen Kiama ataendelea kuhudumu kama Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) baada ya mahakama kukataa ombi la Waziri wa Elimu George Magoha la kutaka uteuzi wa Kiama ufutiliwe mbali.

Waziri Magoha aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Masuala ya Ajira na Mahusiano ya Leba akitaka uteuzi wake wa Profesa Isaac Mbeche kama kaimu Naibu Chansela udumishwe.

Alisema Jaji wa mahakama hiyo, Maureen Onyango, alipotoshwa na Profesa Kiama alipotoa amri kwamba aendelee kuhudumu kama Naibu Chansela baada ya kuteuliwa na Baraza la Chuo hicho chini ya uongozi wa Profesa Julia Ojiambo.

Lakini Alhamisi, Jaji Onyango ameamuru kuwa kesi hiyo isikizwe Ijumaa katika kikao ambapo wawakilishi kutoka pande zote inatarajiwa watahudhuria. Aliorodhesha kesi hiyo kama ya dharura.

Kwenye kesi aliyowasilisha, Magoha alisema kuwa wadhifa wa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi bado uko wazi.

“Mahakama inafaa kuondoa amri iliyotoa Jumatatu ili Waziri aweze kuteua naibu Naibu Chansela na Msaidizi wa Naibu Chansela ili chuo kiweze kuendelea na shughuli muhimu za usimamizi. Mahakama isipotoshwe na Prof Kiama kwamba yeye ndiye mkuu wa taasisi hiyo,” zikasoma stakabadhi ambazo waziri aliwasilisha mahakamani na wakili wa Profesa Magoha ambaye ni Evans Monari.

Profesa Magoha alisema amri ya Jaji Onyango iliyotolewa Jumatatu itaathiri utendekazi wa chuo, wakati huu ambapo kuna pengo katika afisi ya Naibu Chansela na baraza la chuo hicho.

“Licha ya kuwepo kwa pengo hilo, Prof Kiama ameendelea kujiwasilisha kama Naibu Chansela na kufanya mabadiliko makubwa kuhusu usimamizi wa chuo na kuhadaa umma,” akasema wakili Monari.

Mnamo Jumatatu mahakama hiyo ilisitisha uamuzi wa waziri Magoha wa kubatilisha uteuzi wa Profesa Kiama kama Naibu Chansela.

Jaji Onyango alitoa uamuzi huo baada ya Profesa Kiama kuwasilisha kesi ya kupinga hatua ya Profesa Magoha kufutilia mbali uteuzi wake na badala yake kumteua Profesa Isaac Mbeche kama Kaimu Naibu Chansela.

Kufikia sasa Profesa Kiama ametangaza teuzi mpya katika taasisi hiyo, na kumtuma Profesa Mbeche kwa likizo.

Katika taarifa aliyotoa Januari 21, 2020, Profesa Kiama alimteua Profesa Madara Ogot, ambaye ni Msaidizi wa Naibu Chansela (DVC) anayesimamia Utafiti, kuwa kaimu Msaidizi wa Naibu Chansela anayesimamia Masuala ya Fedha.