• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Uhuru aadhibu wasiofuata nyayo zake

Uhuru aadhibu wasiofuata nyayo zake

Na WANDERI KAMAU

WANASIASA ambao wanakosa kufuata nyayo za Rais Uhuru Kenyatta wanapitia kipindi kigumu kwa misimamo yao ya kisiasa, na pia ujasiri walio nao wa kumkosoa.

Katika kile kimejitokeza kuwa sifa ya kutopenda kupingwa na yeyote, Rais Kenyatta anafanya kila juhudi kuzima wakosoaji wake.

Hii ni kufuatia hatua ya Rais Kenyatta, wanasiasa wa mrengo wa Kieleweke na maafisa serikalini kuchukua hatua kali kuwanyoosha wale ambao wanaonekana kama waasi dhidi ya rais.

Wanasiasa hao wamekuwa na wakati mgumu hasa katika hafla za rais kwa kufukuzwa ama kukatazwa kuhutubu mbali na mahangaiko mengine.

Wengi wa wanasiasa ambao wameona moto ni wabunge wa chama cha Jubilee kutoka ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta katika Mlima Kenya, ambao amekuwa akiwakashifu vikali kila mara anapokuwa kwenye hafla eneo hilo.

Kwenye ziara ambazo amekuwa akifanya katika kaunti kadhaa za Mlima Kenya wabunge waasi wamekuwa wakizuiwa kuingia ama kuhutubu kwenye mikutano yake.

Mwezi uliopita, Seneta Susan Kihika wa Nakuru na mbunge David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki) walizuiwa kuingia kwenye hafla iliyoongozwa na Rais Kenyatta katika utoaji wa hatimiliki kwa wanawake wa kundi la Nyakinyua.

Kufuatia kisa hicho, wabunge wote wanane wa Kaunti ya Nakuru walisusia hafla ya rais katika eneo la Molo wiki iliyopita kwa hofu ya kuaibishwa kwa kufukuzwa kama ilivyowatokea wenzao Bi Kihika na Bw Gikaria.

Baada ya hafla hiyo Rais Kenyatta alielekea Bahati ambako alimkashifu vikali mbunge wa eneo hilo Kimani Ngunjiri kwa kugeuka mkosoaji wake mkuu.

Katika Kaunti ya Nyandarua alikozuru rais Ijumaa iliyopita, wabunge Faith Gitau (Mwakilishi wa Wanawake), Michael Muchira (Ol Joro Orok), Kwenya Thuku (Kinangop) na David Kiaraho (Ol Kalou) walikatazwa kuhutubu.

Kwenye ziara yake katika Kaunti ya Kirinyaga mnamo Jumamosi, wabunge Munene Wambugu (Kirinyaga ya Kati), Kabinga wa Thayu (Mwea) na Gichimu Githinji (Gichugu) pia walijipata kwenye baridi waliponyimwa fursa ya kuhutubu.

Hayo yakijiri siku hiyo ya Jumamosi, Mbunge wake Rais Kenyatta katika eneo la Gatundu Kusini, Moses Kuria alikuwa akihangaishwa kwenye mkutano wa BBi mjini Kitui kwa kile agizo la Gavana Charity Ngilu aliyesema ana mazoea ya kumkosea heshima rais.

Bw Kuria alikuwa wa kwanza mnamo 2018 kumkosoa rais akidai amekosa kupeleka maendeleo eneo la Mlima Kenya, hali aliyosema imeongeza umaskini miongoni mwa wakazi.

Mwezi uliopita Rais Kenyatta alijibu shutuma za wabunge hao waasi kwa kutangaza hatua za kufufua uchumi wa Mlima Kenya hasa kilimo cha kahawa, majani chai na kahawa.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua amesema wanasiasa wanaoonekana kutofuata nyayo za rais sio waasi mbali wamekuwa wakimwambia ukweli kuhusu matatizo yanayowakumba wananchi.

“Kama tungenyamaza rais hangejua kuhusu matatizo ambayo watu wetu wanapitia. Sisi hatuikosoi serikali mbali tunaeleza vile hali ilivyo,” akasema Bw Gachagua.

Rais pia amekuwa akionyesha hadharani kuchoshwa na wakosoaji wake. Mnamo Februari mwaka uliopita aliondoka kwa muda jukwaani wakati Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro alipoamka kuhutubu kwenye mazishi ya mfanyabiashara Kamau Thayu.

Mnamo Desemba mwaka jana, mbunge huyo alikuwa miongoni mwa viongozi ambao rais alikosa kuwasalimia kwa mkono wakati wa mazishi ya mwanasiasa Charles Rubia.

Wakosoaji hao waasi pia wamelalamika kuhangaishwa na serikali kwa kunyang’anywa walinzi ama kufunguliwa mashtaka.

Mnamo Novemba, Bw Nyoro alikamatwa baada ya kizaazaa kuzuka kati yake na mbunge maalum Maina Kamanda kwenye hafla moja ya kanisa Murang’a.

Bw Kuria pia alikamatwa mwezi uliopita akidaiwa kupigana kwenye studio za Royal Media Services.

Wiki iliyopita, Bw Ngunjiri aliagizwa kurudisha bunduki yake.

Hata hivyo, mchanganuzi wa siasa Prof Macharia Munene amemtetea Rais Kenyatta, akisema kuwa viongozi wanapaswa kumpa muda kutimiza ahadi alizowapa Wakenya.

You can share this post!

Arsenal sasa majogoo wa kulazimisha sare

DPP aomba mwezi mmoja zaidi katika kesi ya Cohen

adminleo