Mbunge ataka siasa za 2022 zikomeshwe
Na KALUME KAZUNGU
MBUNGE wa Lamu Magharibi, Athman Sharif (pichani), anasema makubaliano ya pamoja ya utendakazi kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani (NASA), Raila Odinga yatakuwa na manufaa iwapo viongozi na wafuasi wa wawili hao wataacha kuzozana kuhusu siasa za 2022.
Akizungumza na Taifa Leo Ijumaa, Bw Sharif alitaja maafikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuwa kuwa changizo kubwa iliyopelekea amani na utulivu kujiri hapa nchini.
Bw Sharif aliwaonya wanasiasa na wafuasi wa wawili hao dhidi ya kukiuka ajenda za maafikiano ya Uhuru na Raila na kutumia mwanya huo kuendeleza siasa zisizo na mwelekeo wowote.
Aliwataka viongozi na wafuasi wa mirengo miwili ya Jubilee na NASA kushirikiana vilivyo na kufanya kazi ili kuleta maendeleo hapa nchini.
Pia aliwataka wanasiasa ambao tayari wameanza kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kujipigia debe ya uchaguzi mkuu ujao wa 2022 kukoma kufanya hivyo.
“Nimefurahishwa sana na kuja pamoja kwa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Punde wawili hao walipotupilia mbali tofauti zao na kuja pamoja, hata uchumi wan chi wenyewe uliimarika kuanzia hapo.
Ombi langu kwa viongozi hasa wa kisiasa na wafuasi wao ni kwamba waache kampeni za 2022. Tushirikiane kwa kufanya kazi pamoja ili kufanya makubaliano ya wawili hao kuwa ya maana,” akasema Bw Sharif.