• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Raila akamilisha ziara ya kumwakilisha Uhuru Afrika Kusini

Raila akamilisha ziara ya kumwakilisha Uhuru Afrika Kusini

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga anatarajiwa kurudi nchini leo baada ya ziara rasmi ya kumwakilisha Rais Uhuru Kenyatta kwenye mazishi ya Winnie Mandela Afrika Kusini.

Mbali na hafla hiyo ya mazishi, Bw Odinga jana alikuwa amepengiwa kuwa na mkutano wa kibinafsi na Rais Cyril Ramaphosa.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, mshauri wake Bw Silas Jakakimba, alisema mkutano huo ulikuwa wa kibinafsi.

“Mheshimiwa Raila Odinga atakutana na Rais Cyril Ramaphosa kabla ya kurejea Kenya. Mkutano huo utakuwa na kibinafsi,” akasema Bw Jakakimba ambaye alikuwa katika ujumbe wa kiongozi huyo.

Bw Odinga anatambuliwa kuwa na urafiki na viongozi kadhaa wa Afrika, akiwemo Bw Ramaphosa ambaye alichukua uongozi majuzi kutoka kwa aliyekuwa rais Jacob Zuma.

Alipowasili Afrika Kusini siku ya Ijumaa, kiongozi huyo wa chama cha ODM ambaye sasa anashirikiana na Rais Kenyatta, alilakiwa na Balozi wa Kenya nchini humo Bi Jean N Kamau na maafisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Afrika Kusini.

Kiongozi huyo aliandamana na mkewe, Ida, bintiye Winnie Odinga na Seneta wa Kisii Profesa Sam Ongeri.

Winnie, ambaye alishiriki katika mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo, alikuwa mkewe Rais wa kwanza mweusi nchini humo shujaa Nelson Mandela. Alizikwa Jumamosi katika hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya watu pamoja na wageni kutoka mataifa ya nje.

Katika risala yake ya rambirambi, Bw Odinga alisema daima marehemu Winnie atakumbukwa na wale ambao walishuhudia na kufaidi kutokana na juhudi zake na kupinga utawala dhalimu wa mbeberu.

“Alijitolea mhanga kwa ajili ya ukombozi wa Afrika Kusini na watu wake. Na akapoteza mengi kama mtu binafsi. Lakini nafasi yake katika historia ni thabiti kwa mashujaa na wahasiriwa ulimwenguni,” akasema Bw Odinga.

Wakati wa ibada ya ukumbusho iliyoandaliwa katika uwanja wa michezo wa Orlando mjini Soweto, Bw Odinga alikutana na Naibu Rais wa Afrika Kusini David Mabuza, Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa Lindwe Sisulu, Rais wa zamani Thabo Mbeki, miongoni mwa viongozi wengine mashuhuri.

Bi Mandela aliyefariki Aprili 2 akiwa na umri wa miaka 81 alizikwa katika bustani ya Four Way Memorial jijini Johannesburg.

Hapo ndipo mjukuu wake, Zenani Mandela alizikwa mnamo 2010 alipofariki baada ya kugongwa na gari.

Kumwakilisha rais kwenye hafla hiyo muhimu ya kitaifa kunaonekana kuwa sehemu ya matunda ya ushirikiano wa Bw Odinga na Bw Kenyatta, ambaye alikuwa mpinzani wake mkuu kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 mwaka jana.

Lakini tangu wasalimiane hadharani Machi 9 mwaka huu, mambo yamebadilika.

You can share this post!

Malori yenye magunia 330 ya makaa yanaswa

Marufuku kutafuna miraa na muguka Nyandarua

adminleo