Marufuku kutafuna miraa na muguka Nyandarua
Na WAIKWA MAINA
WATAFUNAJI wa miraa na muguka katika Kaunti ya Nyandarua sasa watalazimika kutafuta bidhaa hizo katika kaunti jirani kama vile Nakuru na Laikipia baada kupigwa marufuku katika kaunti hiyo.
Maafisa wa usalama walipiga marufuku uuzaji na utumiaji wa miraa na muguka katika maeneo yote ya vijijini kwenye kaunti hiyo.
Miraa ilipigwa marufuku baada ya wakazi wa wilaya ya Nyandarua ya Kati waliokongamana katika shule ya msingi ya Kandutura kulalama kuwa maeneo ya kuuza miraa na muguka yamegeuka kuwa maficho ya wahalifu. Wakazi pia walisema utafunaji wa miraa na muguka umechangia katika watoto kuachana na masomo.
Walisema vijana ambao ni waraibu wa miraa wamekuwa wakiiba vitu mbalimbali kama vile masufuria, mayai, mahindi na viazi ili kupata fedha za kununua bidhaa hiyo. Wakazi walisema kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaoacha shule na kujiunga na uraibu wa miraa.
Walilalama kuwa wauzaji wa miraa wanacheza muziki unaokiuka maadili kwa lengo la kuwavutia vijana. Naibu Kamishna wa Kaunti Gideon Oyagi aliagiza polisi kuvamia vibanda vya kuuza miraa na muguka.
“Nimesikia wauzaji wa miraa wakisema kuwa wanataka kuhamia katika maeneo ya mijini. Lakini ninawaonya kuwa sitaki kuwaona katika eneo ninalosimamia. Waende kwingineko,” akasema Bw Oyagi.
Naibu wa Kamishna pia aliagiza machifu na manaibu wao kuandaa mipango ya utoaji ushauri nasaha kwa watoto ambao wameathiriwa na utafunaji wa miraa.
Mwezi uliopita, Bunge la Kaunti ya Kwale lilipitisha hoja ya kupiga marufuku biashara ya miraa na muguka katika eneo hilo.
Madiwani walisema wengi wa vijana walikatazwa kujiunga na jeshi la KDF kutokana na vigezo kwamba walikuwa na dosari zinazosababishwa na utafunaji wa miraa na muguka.