Echesa kukaa rumande mpaka Jumatatu kwa sakata ya Sh40b
Na FRANCIS NDERITU
ALIYEKUWA Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa, Ijumaa alitupwa rumande na mahakama moja jijini Nairobi hadi Jumatatu jioni ili kuwapa polisi nafasi ya kumaliza uchunguzi dhidi ya mashtaka yanayomkabili.
Mahakama iliagiza kuwa Bw Echesa ataachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni baada ya polisi kumaliza uchunguzi wao.
Bw Echesa alikamatwa mnamo Alhamisi na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Mashtaka ya Jinai (DCI) kuhusiana na sakata ya tenda ya vifaa vya kijeshi vyenye thamani ya Sh40 bilioni.
Alifikishwa katika Mahakama ya Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), ambapo polisi walimwomba hakimu kuwaruhusu kumzuilia kwa siku 21 ili kumaliza uchunguzi.
Upande wa mashtaka ulisema kwamba wachunguzi wanahitaji kusafiri nchini Amerika kukusanya ushahidi zaidi.
Mahakama pia iliambiwa kuwa kumwachilia kutahatarisha ukusanyaji wa ushahidi.
Hata hivyo, wakili wake, Bw Evans Ondieki alipinga ombi hilo, akisema kuwa kukamatwa kwake kumechochewa na sababu za kisiasa. Pia alisema kuwa kuna njama fiche, ikizingatiwa wakati aliokamatwa na muda ambao upande wa mashtaka unataka kumzuilia.
Mahakama iliwaruhusu polisi kumzuilia Bw Echesa na washukiwa wengine, ambapo pia watafanya uchunguzi majumbani mwao. Bw Echesa atazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga.