Maelfu kwenye mafuriko wahitaji msaada wa dharura
Na WAANDISHI WETU
MAELFU ya Wakenya katika maeneo mbalimbali ya nchi wanahitaji msaada baada ya makazi na mazao yao kusombwa na mafuriko.
Katika Kaunti ya Kisumu, zaidi ya watu 2,000 kutoka eneobunge la Muhoroni wanahitaji msaada kwa dharura baada ya makazi na mali yao kusombwa na mafuriko yaliyotokana na kupasuka kwa kingo za Mto Nyando, Jumamosi.
Idadi ya waathiriwa imekuwa ikiongezeka katika kambi za muda za kupokea manusura zilizowekwa katika maeneo ya Mitandi, Achuodho na Katundu katika Wadi ya Ombeyi.
Mafuriko hayo ya Jumamosi yalisomba nyumba na mifugo.
Wanaume waliojistiri katika eneo la Katundu jana walilazimika kulala nje ya hema ambapo zaidi ya waathiriwa 500 wametafuta hifadhi. Ni wanawake na watoto tu walioruhusiwa kulala ndani ya hema.
Waathiriwa walisema Mto Nyando ulivunja kingo zake Jumamosi mchana kufuatia mvua kubwa na kusababisha mafuriko.
Sasa kuna wasiwasi kuwa waathiriwa hao huenda wakashikwa na maradhi kama vile malaria, kichocho, kipindupindu na magonjwa mengineyo.
Katika Kaunti ya Isiolo, nyumba kadhaa zilisombwa na mafuriko katika vijiji vya Baasa na Malkagala kwenye wadi ya Cherab na kuwaacha wanakijiji bila makazi.
Naibu Kamishna wa Wilaya ya Merti Julius Maiyo alisema hajapata idadi kamili ya waathiriwa.
Katika Kaunti ya Kisii, wakulima walipata hasara baada ya Mto Kuja kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko yaliyosomba mazao.
Mkazi wa eneo la Mugirango Kusini Thomas Gigoye, alisema mafuriko hayo yaliharibu mashamba ya ndizi katika eneo hilo.
Mjini Kisii, madereva na wahudumu wa bodaboda wanataka kujengwa kwa daraja litakalounganisha eneo la mjini na mtaa wa Jogoo.
Ripoti za Victor Otieno, Rushdie Oudia, Vivian Jebet na Magati Obebo