Habari Mseto

Raila, Ruto kukaa jukwaa moja mkutano wa BBI

February 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

GITONGA MARETE na WANJOHI GITHAE

MACHO yote yataelekezwa Meru Jumamosi ijayo Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM watakapokutana katika mkutano ujao wa uhamasisho kuhusu mpango wa maridhiano (BBI) utakaofanyika katika uwanja wa Kinoru mjini Meru.

Hii ndio itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili, ambao ni mahasidi wa kisiasa, kushiriki jukwaa moja la kisiasa tangu Dkt Ruto alipogura ODM mnamo 2008. Hata hivyo, wamekuwa wakikutana mara kadha katika sherehe za kitaifa na hafla za mazishi.

Awali, Dkt Ruto amewahi kudai kuwa mikutano ya BBI ni majukwaa ya ODM yanayolenga kuchapa siasa za mwaka wa 2022 na uwepo wake katika mkutano wa BBI Meru utawafanya waandalizi kujikuna vichwa hasa kuhusiana na suala la itifaki.

Mpango wa BBI ulianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga na hiyo ndio maana katika mikutano ya uhamasisho, kiongozi huyo wa ODM ndiye huongea wa mwisho, alivyofanya Jumamosi mjini Narok.

Lakini Bw Odinga anasisitiza kuwa mikutano hiyo ni wazi kwa kila mtu kwani ni majukwaa ya kujadili masuala ya kuboresha taifa hili.

Naibu Msemaji wa Dkt Ruto, Emmanuel Tallam alithibitisha kuwa kiongozi huyo atahudhuria mkutano wa BBI uwanjani Kinoru.

Hata hivyo, alifafanua kuwa chama cha Jubilee kimekuwa kikijadiliana kuhusu idadi ya mikutano ya BBI ambayo Dkt Ruto atahudhuria.

“Ndio, Naibu Rais atahudhuria mkutano wa BBI katika kaunti ya Meru lakini Jubilee inajadiliana kuhusu suala hilo,” akasema Tallam.

Na Alhamisi wiki iliyopita, Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alitangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba Dkt Ruto atashiriki jukwaa moja na Bw Odinga, Meru.

“Mkutano wa BBI mjini Meru mnamo Februari 29, utakuwa mzuri zaidi kwa sababu utahudhuriwa na Naibu Rais Dkt Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa pamoja. Hii ndiyo Kenya tunayoitaka,” Bw Kuria aliandika.

Wakati huu, Dkt Ruto anaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge kutoka eneo hilo la Mlima Kenya na amekuwa akihudhuria hafla nyingi za kidini.

Rais Kenyatta ambaye alizuru eneo hilo majuma mawili, hajawahi kuhudhuria mikutano hiyo na huenda asihudhurie mkutano wa Meru, Jumamosi.

Mnamo Ijumaa mkutano wa wajumbe kutoka kaunti 11 watahudhuria. Wataandaa mapendekezo yao ambayo yatawasilishwa katika mkutano wa hadhara uwanjani Kinoru. Mapendekezo ya wajumbe wa maeneo mbalimbali yamekuwa yakiwasilishwa kwa Bw Odinga na wanachama wa jopo kazi la BBI.

Tayari, kaunti za Meru, Tharaka Nithi na Embu zimefanya mikutano yao na ziko tayari kwa mkutano mkubwa wa BBI mjini Meru.

Kaunti zingine ambazo zinatarajiwa kufanya mikutano yao wiki hii ni Kirinyaga, Laikipia, Nyeri, Nyandarua, Nakuru, Nairobim, Muranga, na Kiambu.

Gavana wa Meru ambaye atakuwa mwenyeji wa mikutano ya Ijumaa na Jumamosi, alisema hawajaafikiana kuhusu idadi ya wajumbe watakaohudhuria mkutano wa Ijumaa.

“Mashauriano bado yanaendelea lakini tunatarajia kaunti zote kuwakilishwa katika mkutano wa Ijumaa,” akasema Bw Murungi. Hata hivyo, alikataa kusema ni nani atagharamia mikutano hiyo.

Eneo la Mlima Kenya ni ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta lakini limegawanyika kisiasa baada ya kuchipuza kwa mirengo ya Tangatanga na Kieleweke ndani ya Jubilee.