Habari Mseto

Sonko atimua kaimu katibu

February 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi anayekabiliwa na kesi kortini, Mike Sonko amemwachisha kazi Kaimu Katibu wa Kaunti, Bw Leboo Morintat.

Wawili hao walikuwa wandani kwa muda mrefu, hadi pale Bw Morintat alianza kuwasilisha stakabadhi za kaunti kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kila anapoagizwa na maafisa wa kuchunguza ufisadi kufanya hivyo.

Haijajulikana wazi kama Bw Morintat anachukuliwa kama shahidi au mshukiwa kuhusiana na kashfa zinazochunguzwa.

Nafasi ya Bw Morintat sasa itashikiliwa kwa muda na Afisa Mkuu wa Mipango wa Mji, Bw Justus Kathenge.

Bw Kathenge alirudi katika serikali ya kaunti mwezi uliopita kama afisa mkuu wa Upangaji wa Mji baada kusimamishwa na Gavana Sonko mnamo Agosti 2019.

Bw Morintat alikuwa akimtetea Bw Sonko, pamoja na kuongoza mikutano katika serikali ya kaunti tangu Gavana aagizwe kutoingia afisini mwake mwaka 2019.

Kuonyesha jinsi wawili hao walivyokuwa karibu, mnamo Septemba 2018 Bw Sonko alibuni nafasi ya naibu katibu wa kaunti – cheo ambacho hakitambuliwi kisheria – ikasimamiwa na Bw Morintat.

Lakini uhusiano kati yao umetatizwa na uchunguzi wa mara kwa mara katika Jiji la Nairobi na wapelelezi.

Wakati wa uchunguzi huo, Bw Morintat ameitwa katika mikutano kadhaa kuandikisha taarifa na kutoa hati kuhusu suala hilo.

Bw Sonko anakumbwa na masaibu tele ikiwemo kesi ya ufisadi iliyosababisha agizo la kumzuia asiingie afisini mwake katika makao makuu ya kaunti, na madiwani wameanzisha mchakato wa kutaka ang’olewe mamlakani.

Wiki iliyopita, ilani ya kuwasilisha hoja ya kumwondoa mamlakani ilipelekwa katika bunge la kaunti na kiongozi wa wachache Bw Peter Imwatok.

Hii si mara ya kwanza kwa Bw Sonko kutimua maafisa wa serikali yake ambao huonekana kwenda kinyume na matarajio yake.

Mwezi uliopita, alimsimamisha kazi Waziri wa Fedha katika kaunti, Bi Pauline Kahiga kuhusu ulipaji wa madeni yanayofika Sh1.4 bilioni ambayo kaunti inadaiwa.

Juhudi zake za awali kumtimua waziri huyo zilikuwa zimegonga mwamba. Alijaribu kujaza nafasi hiyo kwa kumteua Bw Allan Igambi, lakini serikali kuu ikakataa kuchapisha mabadiliko hayo kwenye gazeti rasmi la serikali.

Suala hilo sasa liko mbele ya Mwanasheria Mkuu, ijapokuwa dalili zaonyesha Bi Kahiga angali ana mamlaka katika Wizara ya Fedha ya kaunti.

Wiki iliyopita, Bi Kahiga aliidhinisha ulipaji wa Sh166.9 milioni kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa nchini (KEMSA).

Alisema Sh120 milioni zitatumiwa kugharamia madeni ambayo KEMSA inadai serikali ya kaunti, huku Sh46 milioni zikitumiwa kwa ununuzi wa dawa mpya zitakazosambazwa kwa hospitali za kaunti.